Rasmi Uongozi wa Klabu ya Singida Big Stars umefanya masahihisho kwenye Logo yake, kwa lengo la kulinda historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2010.
Mabadiliko hayo yamekuja baada ya kuibuka kwa mkanganyiko wa muda sahihi wa kuanzishwa kwa Klabu hiyo, ambayo ilitambulika kwa jina la DTB wakati ikishiriki madaraja ya chini kabla ya kupanda Ligi Kuu msimu wa 2022/23.
Logo ya awali ilionesha Singida Big Stars imeanzishwa mwaka 2021, lakini ukweli ni kwamba ilipaswa kuonesha mwaka 2010.
“Historia ya Singida Big Stars inaanzia DTB FC kabla ya kubadilishwa jina. Mwaka 2021 ni mwaka tulipobadili jina kutoka DTB FC kwenda Singida Big Stars” imeeleza taarifa ya Klabu hiyo
Uongozi wa Klabu ya Singida Big Stars iliinunua klabu ya DTB mwishoni mwa msimu uliopita (2021/22), siku chache baada ya kumalizika kwa Ligi ya Championship, na kuhamishiwa mjini Singida ikitokea jijini Dar es salaam.
Kwa sasa Singida Big Stars ni moja ya klabu zinazofanya vizuri katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi kuu, ikiwa na alama 37.
Pia imeshiriki kwa mara ya Kwanza Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023, na kufika hatua ya Fainali kaya kupoteza dhidi ya Mlandege FC kwa kufungwa 2-1, Ijumaa (Januari 13).