Singida BS yawagomea Kagere na Wawa



BENCHI la ufundi la Singida Big Stars, limesema licha ya ofa zilizopo kwa baadhi ya nyota wao, lakini halitakubali kuwaruhusu mastaa waliosajiliwa kimkakati akiwamo straika, Meddie Kagere na beki Pascal Wawa wote kutoka Simba.

Timu hiyo ambayo imeanza kuongeza nguvu kwa kumsajili winga wa kushoto, Nickson Kibabage, kutoka Mtibwa Sugar, imeonekana kuwa imara kwenye ligi kuu ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 30 ikizidiwa na vigogo wa soka nchini, Yanga, Simba na Azam zote za jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa benchi la ufundi la timu hiyo, Ramadhan Nswanzurimo aliliambia Mwanaspoti kuwa timu hiyo ina mikakati na malengo yao ndio maana waliamua kuwa na mastaa wakubwa ili kuitangaza klabu yao hivyo hawatakuwa tayari kuruhusu nyota hao kuondoka.

Alisema Singida Big Stars iliamua kuvunja benki kupata nyota wa maana ambao hata matokeo waliyonayo hivi sasa ni kutokana na usajili bora walioufanya hivyo hawana mpango wa kumuacha yeyote bali kuongeza.


“Umuache mtu kama Kagere au Wawa unakuwa na malengo gani? Alihoji na kuongeza; “Ofa zipo nyingi lakini hatupo tayari, huyu Kagere ndiye staa wetu kikosini ndio maana muda wote tuko naye karibu hata juzi kwenye mechi ya Tanzania Prisons alipokosa bao tulimuita pembeni na kocha mkuu, Hans van Pluijm kumuweka vizuri kisaikolojia.”

Alisema tangu nyota huyo atue kikosini amekuwa na kiwango bora na kuwaongoza wenzake vyema jambo ambalo linawapa nguvu benchi la ufundi na kwamba mabao matano aliyonayo kwa sasa si haba na anaweza kuzidi idadi hiyo.

“Ukiachana na Yanga na Simba, Singida Big Stars ndio timu kubwa inayofuata hivyo hatuwezi kuwa nyuma kwenye mbio za ubingwa, kwa ujumla tunafurahia kiwango chetu.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad