BAADA ya kuanza kuitumikia Yanga, straika mpya wa timu hiyo, Mzambia, Kennedy Musonda, ameweka wazi kuwa anajua miongoni mwa michezo mikubwa hapa nchini ni Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba na kuweka wazi kuwa ana shauku kubwa ya kuwafurahisha Yanga hususani katika mchezo huo.
Musonda ni miongoni mwa mastaa watatu wapya ambao wamesajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo la usajili, huku akikamilisha usajili wake na kutangazwa rasmi usiku wa Ijumaa iliyopita akijiunga kutokea ndani ya kikosi cha Klabu ya Power Dynamos ya Zambia.
Staa huyo aliichezea Yanga mchezo wake wa kwanza Jumatatu wiki hii dhidi ya Ihefu, ambapo alitumika kwa dakika 27 wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.
Akizungumzia mchezo wake wa kwanza ndani ya Yanga, Musonda alisema: “Nashukuru kwa kufanikiwa kupata nafasi ya kucheza mchezo wangu wa kwanza ndani ya Yanga, kocha kwa kuniamini licha ya kwamba nilikosa sehemu kubwa ya maandalizi ya mchezo.
“Nilikuwa na nyakati nyingi nzuri nikiwa Zambia na kupata nafasi ya kucheza michezo mingi hususani ile mikubwa ya dabi, najua hapa Tanzania kuna dabi kubwa ya Yanga na Simba ambayo ni miongoni mwa dabi bora za Afrika, nina shauku kubwa ya kucheza mchezo huo na kuwafurahisha mashabiki.”
STORI NA JOEL THOMAS