KAMATI ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetoa ruhusa kwa kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwenda kushitaki katika Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Soka ya Kimataifa (Cas).
Hiyo ikiwa saa chache mara baada ya kamati hiyo, kutoa hukumu ya sakata lake la kuvunja mkataba wake wa miaka miwili alioubakisha Yanga.
Kamati hiyo, juzi Jumamosi ilitoa hukumu ya kiungo huyo kuwa inamtambua ni mali ya Yanga baada ya kupitia mikataba ya pande zote mbili.
Akizungumza na moja ya kituo cha Radio kikubwa hapa nchini, Mwenyikiti wa kamati hiyo, Said Sudi alisema kuwa Fei Toto ni mchezaji halali wa Yanga na baada ya kuupitia mkataba wake na kuonyesha wazi ni mali yao.
Sudi alisema kuwa wanatoa nafasi kwa kiungo huyo kwenda mbali zaidi na sio kurudi tena kwao TFF, ikiwemo CAS na wapo tayari kumpa review ili aende huko.
“Mkataba unaonyesha wazi ni mali ya Yanga, ila kama Fei Toto hajaridhika na maamuzi yetu anayo nafasi ya kukata rufaa na sisi tutampa review aende CAS sio hapa tena.
“Kwani hapa kwetu tayari hilo suala tumelimaliza, kwa kumuidhinisha ni mchezaji wa Yanga mwenye mkataba wa kuichezea timu yake hiyo,” alisema Sudi.
Kwa upande wa wakili wa kiungo huyo, Nduruma Majembe alizungumzia hilo kwa kusema: “Mteja wangu (Fei Toto) hana tena mapenzi ya kurudi na kuendelea kuitumikia klabu yake ya Yanga.
“Kwani katika kikao cha kamati aliweka dhahiri kwamba hakuna uwezekano wa yeye kurudi tena kuichezea Yanga. Labda atafutiwe mwanasaikolojia atakayebadilisha mawazo yake.
“Nikiri kupokea kwa taharuki na masikitiko makubwa maamuzi ya kamati dhidi ya Fei Toto kumrejesha Yanga, na ifikapo Jumatatu (leo) tutajua sababu ambazo kamati zimefanya kumbakisha Yanga, lakini pia tunaweza kuomba review ya hukumu au kwenda moja kwa Moja CAS kupinga maamuzi hayo,” alisema Majembe.
STORI NA WILBERT MOLANDI