Ujazwaji maji bwawa la Julius Nyerere wafikia mita 108

 


Dar es Salaam. Ujazo wa maji katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) linalotarajiwa kujaa ndani ya miezi 18 hadi jana ulifika mita 108.31 kutoka usawa wa bahari.

Ujazaji maji katika bwawa hilo linalotarajiwa kuzalisha megawati 2,115 za umeme likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 32 ulianza Desemba 22 mwaka jana.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Wadau wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Elihuruma Ngowi alisema bwawa linaendelea kujaa kwa kasi kwa sababu yamejikusanya kwenye eneo dogo.

“Muda wa kujaa bado ni uleule yaani misimu miwili ya mvua. Mita zinaonekana ziko juu kwa sababu maji yamejaa sehemu moja, lakini yakianza kusambaa maeneo mengi, zitakuwa zinakwenda taratibu,” alisema Ngowi.

Wakati maji ya masika ya mwaka na mwakani yakiendelea kujaa, alisema shughuli nyingine za ujenzi zinaendelea.

“Ujenzi hautosimama, mwenendo wa bwawa kujaa maji ni mzuri,” alisema Ngowi.

Siku ya ujazwaji maji, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande alisema wamejenga tuta lenye urefu wa mita 131 kwenda juu huku bwawa lenyewe likiwa na urefu wa kilomita 100 sawa na kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze.

Ujenzi wa njia za kuporomosha maji alisema umekamilika kwa asilimia 96 na mahandaki matatu yenye mashine zitakazotumika kuzalisha megawati 235 kila moja, yana urefu tofauti, moja likiwa na urefu wa mita 390, jingine 440 na 520.

“Maji yanayopita katika njia moja ya mashine hizo ni lita 200 kwa sekunde, ni mradi mkubwa sana,” alibainisha.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad