Utepe wa noti za 2,000 wageuka dili kwa 'mateja'



Dar es Salaam. Mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini bado yanakabiliwa na changamoto baada ya kuibuka mbinu mpya ya ulevi unaohusisha utepe wa noti ya Sh2,000, Mwananchi limebaini.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini uharibifu huo unahusisha uvutaji wa moshi wa madini yanayochunwa katika utepe wa noti hiyo, moja ya alama muhimu za utambulisho wake, ingawa haipotezi thamani.

Matumizi ya utepe huo yanayofahamika kama kuvuta bamba, yanaelezwa kuwa wa gharama nafuu ukichangiwa na kupungua kwa upatikanaji heroine kutokana na udhibiti mkali wa mamlaka za Serikali.

“Inabidi upate noti mpya kuutoa huo utepe, ukiupata unauchubua kutoa madini fulani ambayo unachoma halafu unauvuta moshi wake kwa kutumia mrija mwembamba wa utepe huo baada ya kuuchuna,” anasema mmoja wa watumiaji kutoka Temeke.


Mkuu wa Kitengo cha Kinga na Mafunzo wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma kilicho chini ya Wizara ya Afya, Dk Allan Tarimo anasema watumiaji wengi wa dawa za kulevya hufanya hivyo kama mbadala kila wanapokosa pesa za kununua heroine.

“Hiyo bamba ni common (imezoeleka), waligundua ni mbadala. Karibu wote wana-practice (wanatumia),” anasema Dk Tarimo.

Wakati hali ikiwa hivyo mtaani, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema haijapokea taarifa ya uharibifu huo wa kuondoa alama za usalama wa noti.


“Kama kuna tendo hilo ovu, taarifa inatakiwa ielekezwe kwa vyombo vya sheria vitakavyochukua hatua. Uchunguzi unahitajika kubaini kama tatizo hilo lipo. Noti iliyoharibiwa bila kujali kwa makusudi au bahati mbaya haitabadilishwa hadi kitakapopatikana kibali cha Jeshi la Polisi ili kujua imeharibiwa vipi,” ilisema BoT ilipoulizwa.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime alisema taarifa hizo ni mpya. “Kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ufuatiliaji wa kina utafanyika, kwani kama wapo wanaofanya hivyo wanafanya uhalifu wa kuharibu fedha na ni kosa la jinai,” alisema.

Kamanda Misime alisema baada ya Serikali kuongeza jitihada na mikakati ya kudhibiti na kupambana na wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya, mbinu mpya zimetafutwa.

“Ni kama hiyo taarifa inayosema watumiaji wanaharibu baadhi ya noti wakiamini zinaweza kuwasaidia kupata kilevi mbadala, jambo ambalo si kweli,” alisema Misime.


Chanzo cha tatizo

Elemeth Oloo, mratibu wa miradi wa Asasi isiyokuwa ya Serikali ya Peer to Peer iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam anasema matumizi ya utepe huo yalianza kuibuka katika kipindi cha mafanikio makubwa ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

“Heroine ilipokuwa adimu mtaani, waliokuwa addicted (waraibu) wakaanza kutafuta mbadala na kubuni kilevi hicho wakiamini kitasaidia kuwaondolea ‘alosto’. Ni kama mfa maji, atafanya lolote kujisaidia, wanatumia vidonge vya mafua pia,” anasema Oloo.

Kwa miaka 10 iliyopita kuanzia 2011 mpaka 2020, udhibiti wa dawa za kulevya ulifanikiwa zaidi, hasa heroine, cocaine na bangi. Mwaka 2020 kwa mfano, kilo 349.81 za heroine zilikamatwa zikilinganishwa na kilo 55.35 mwaka 2019, mara sita zaidi.

Ingawa bangi ndiyo inaongoza kwa matumizi nchini, mwaka 2014 takwimu zilikadiria kuwapo kati ya watu 250,000 hadi 500,000 walikuwa wakitumia heroine.


“Utepe wa noti ya Sh2,000 sio changamoto kuupata, kuna wapigadebe wakipata chenji anaenda kuibadili apewe noti,” anasema Oloo.

Asasi hiyo inayowaunganisha vijana walioacha kutumia dawa za kulevya, huwashawishi wastani wa waathirika watano kila wiki kuhudhuria kliniki ya methadone, huku ikiwaokoa zaidi ya vijana 500 katika maskani tofauti za Ilala tangu mwaka 2011. “Wapo wengi wanatamani kuacha. Sababu ni kukosa faraja kwa kuona jamii inawatenga,” anasema Oloo.

Baadhi ya vijana walioachana na dawa hizo wanasema matumizi ya utepe yanashawishi, hususan wanapokosa fedha.

“Mie nimevuta sana nikaugua TB, nikaanza matibabu lakini sikujua chanzo. Uvutaji wa bamba ulianza miaka mingi na hauna gharama kubwa, kwani sindano ni Sh500, kama hujui kujidunga unalipa jumla Sh700. Kama sio kukaba au kuuza mwili unatoa wapi?” alisema kijana mmoja.

Ukosefu wa pesa za kununua dawa hizo uliathiri maisha ya Asha Ngambona (49) hivyo akajikuta anauza mwili kabla ya kuambukizwa Virusi vya Ukimwi.


“Ili nipate dawa nililazimika kujiuza, nikagundua nimeathirika mwaka 2008 baada ya kupata ujauzito, mtoto akafariki miezi mitatu baada ya kujifungua,” anasema Asha.

Baada ya kutembelea maskani kadhaa za waraibu, gazeti hili limebaini matumizi ya utepe huo yamepungua ndani ya miaka mitano iliyopita kutokana na hofu ya kupoteza maisha.

Dk Tarimo anasema wameyatembelea zaidi ya maskani 10 kutoa elimu nchini, wakiwatumia watu walioacha kutumia dawa hizo hasa katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Tanga, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam yenye waathirika wengi.

“Wengi kwa sasa wanafanya sniffing (kunusa), hiyo bamba ni common (imezoeleka) na wote wana-practice. Wote tunaowapokea, asilimia 99 tunawaanzishia dawa chini ya uangalizi. Kuhusu TB, ni kweli wengi wanaathirika kwa sababu ya mazingira ya kuambukizana, lishe duni na kudhoofika kwa kinga za mwili,” anasema.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya hakupatikana kulizungumzia hili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad