Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) imemzuia Mfanyabiashara Maryam Shaaban Laurent kutoendelea kufanya biashara ya kuuza bidhaa za Lump Sugar maarufu ‘vipipi’ vinavyodaiwa kutumiwa na Wanawake kujiweka sehemu za siri ili kupata mvuto na kubana maumbile yao.
Katika taarifa yake kwa Vyombo vya Habari, ZFDA imetoa tahadhari ya kutotumika kwa vipipi hivyo huku ikiendelea kufanya msako wa kuviondoa sokoni.
Mkuu wa Divisheni na Vipodozi ZFDA Salim Hamad Kassim amesema wanazichukua sampuli za bidhaa hiyo na kuzipeleka Maabara ili kujiridhisha huku akisema sababu nyingine ya hatari iliyopo kwenye bidhaa hiyo ni kuwa haina lebo, haina ujazo wala ‘expire date’ na vilevile haijulikani imetoka wapi
Mfanyabishara Maryam alipohojiwa ili kuelezea ‘vipipi’ hivyo amesema amekuwa akiviuza kwa njia ya mtandao ——— “Wateja wote nilikuwa najihakikishia kuwa hiki kitu hakina madhara ni cha asili ndicho kilichonitia moyo kufanya hiyo biashara na sitofanya tena hadi vikibainika havina madhara”