WALIMU watatu wa Shule ya Msingi Kakanja katika Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera walionekana kufurahia kitendo cha mwalimu mkuu wa shule hiyo kuwachapa watoto kwenye nyayo, wameamriwa kuhamishwa katika shule hiyo na kupelekwa sehemu nyingine.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila.
Agizo la kuwahamisha lilitolewa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila, kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, baada ya kufika shuleni hapo na kufanya kikao na uongozi na watendaji mbalimbali wa ngazi ya kijiji, kata na wilaya.
Nguvila alisema pamoja na mamlaka nyingine ikiwamo Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo, walimu hao hawapaswi kuendelea kuonekana katika maeneo ya shule hiyo na kuagiza wapelekwe walimu wengine wenye nidhamu nzuri waendelee na majukumu ya kuwafundisha watoto.
"Mkurugenzi pamoja na kuwahamisha walimu hawa kutoka katika hii shule, unapaswa kuendelea kuwafuatilia mwenendo wao na maadili yao katika maeneo ambayo watakwenda, lengo ni kuona kama wamebadilika na wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya ulezi na ufundishaji vyema," alisema Nguvila.
Aidha, alisema madaraka ya Mratibu Elimu, Kata ya Kakanja, Sweetbert Kiiza, yamesitishwa tangu Januari 23, kwa kushindwa kutelekeza wajibu wake kama msimamizi wa elimu na nidhamu katika eneo lake na atapangiwa majukumu mengine.
"Haiwezekani jambo litokee tangu tarehe 10 Januari halafu wewe usiwe na taarifa nalo, lifike kwetu tarehe 23 Januari wakati nikiangalia kwenye kitabu naona umekwishafika hapa shuleni mara tatu, ina maana ulikuja kutalii kwa sababu kama ungekuja kwa ajili ya kukagua na kufanya vikao na walimu, ungechukua hatua haraka, kwa hiyo madaraka yako yamekwisha leo," alisema.
Nguvila alisema kwa kuwa kitendo alichokifanya mwalimu huyo cha kupiga watoto mpaka kuwajeruhi ni cha kijinai, Jeshi la Polisi liendelee na taratibu za kiuchunguzi ili hatua nyingine za kisheria zifanyike.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Stephano Ndabazi, alisema kuwa tukio hilo lilifanyika ndani ya ofisi ya walimu na walioadhibiwa kwa kosa la kutofanya kazi ya mwalimu ni watoto wanne, lakini ni mtoto mmoja aliadhibiwa kawaida katika makalio na wengine watatu wakapigwa kwenye nyayo huku wakiwa wamekanyagwa.
"Katibu tawala tumepokea maelekezo yako pamoja na kwamba kuna hatua zinaendelea kuchukuliwa na haya tunakwenda kuyafanyia kazi, lengo likiwa ni kuhakikisha tatizo kama hili halitokea tena katika shule hii, lakini katika shule nyingine," alisema.
Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Devotha Alexender, alisema siku ya tukio akiwa shuleni hapo alifika ofisini kuwasalimia walimu wenzake na kukuta malalamiko dhidi ya mwalimu mkuu huyo, kuhusu njia aliyoitumia kuadhibu watoto hao.
"Nilikwenda kumweleza mwalimu mkuu namna anavyolalamikiwa na walimu kutokana na njia aliyoitumia kuadhibu watoto hao, akaniambia amenielewa na hatarudia tena kitendo hicho, lakini akaniomba niende kumwombea radhi kwa walimu wenzake kwamba limetokea tu na hatarudia tena," alisema.
Januari 10, mwaka huu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja, wilayani Kyerwa, Issaya Emmanuel, aliwachapa watoto sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo kwenye nyayo za miguu, huku akiwa amewakanyaga kwa mguu wake, kwa kosa la kutofanya kazi (home work) waliyopewa wakati wakienda likizo.
Kutokana na kitendo hicho cha kikatili kilichofanywa na mwalimu huyo, ambaye alipigwa picha na kusambazwa mitandaoni, ameondolewa wadhifa wake wa kuwa mwalimu mkuu na kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi.