Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), limesema wanafunzi 2,095 kati ya 2,180 waliofanya mtihani wa marudio wa darasa la saba uliofanyika kati ya Desemba 21 na 22 mwaka 2022 wamefaulu daraja A hadi C sawa na asilimia 96.1.
Limesema wanafunzi hao kati ya 2,194 waliofutiwa matokeo ya mtihani huo na Necta baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu uliofanyika Oktoba 5, 6 mwaka 2022.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi amesema kati ya wanafunzi 2,194 waliofutiwa matokeo waliofanya mtihani 2,180, wachache hawakushiriki mchakato huo kwa sababu mbalimbali, akisema huenda wengine walikwenda nje ya nchi.
Amasi ameeleza hayo leo Jumatano Januari 4, 2023 wakati akitangaza matokeo ya upimaji wa darasa la nne na mtihani wa kidato cha pili uliofanyika kati ya Oktoba na Novemba 2022.