Dar es Salaam. Uchunguzi mdogo uliofanywa na Mwananchi baada kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne umebaini wanafunzi 1,308 wa shule saba jijini Dar es Salaam wamepata daraja sifuri.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alitangaza watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 522,217 sawa na asilimia 97.66.
Kwenye matokeo hayo, wanafunzi 63,583 sawa na asilimia 12.1 wamepata sifuri na Shule ya Sekondari Mburahati iliyofanya vibaya kwenye mtihani wa kidato cha pili kwa wanafunzi wake 229 kurudia darasa, ipo miongoni mwa zenye wanafunzi wengi waliopata daraja hilo.
Sekondari ya Taifa iliyokuwa na watahiniwa 1,040 waliopata daraja sifuri ni 474, waliopata daraja la nne ni 533 na darala la pili ni wanne tu akiwamo msichana mmoja na wavulana watatu na hakuna daraja la kwanza.
Katika Sekondari ya Mbagala ambayo kwenye mtihani wa kidato cha pili wanafunzi 204 wamerudia darasa, ina wanafunsi 62 waliopata daraja sufuri kidato cha nne kati ya 474 waliofanya mtihani.
Sekondari ya Mburahati ina wanafunzi 116 waliopata daraja sifuri wakiwamo wasichana 45 na wavulana 71 huku wale wa daraja la kwanza hadi la tatu wakiwa 24 na 103 wakipata daraja la nne.
Shule ya Sekondari Kambangwa imeingia kwenye orodha hiyo kwa wanafunzi wake 116 kupata daraja sifuri wanaojumisha wasichana 55 na wavulana 61.
“Wanafunzi waliopata daraja la nne ni 157 na 46 wakiondoka na daraja la kwanza hadi la tatu,” matokeo hayo yaliyopo kwenye tovuti ya Necta yanaonyesha.
Pia, Shule ya Sekondari Pugu Station yenye wanafunzi 201 waliopata daraja sifuri ndio yenye idadi kubwa zaidi katika uchunguzi huo wa Mwananchi ikiwa na wasichana 113 na wavulana 88 waliopata daraja hilo.
Kwenye shule hiyo, idadi ya waliopata daraja la nne ni 251 na wengine 93 wakipata daraja pili na tatu huku ikiwa hana aliyepata daraja la kwanza.
Sekondari ya Chanika iliyopo Wilaya ya Ilala ina wanafunzi 144 waliopata sifuri wakiwamo wasichana 82 na wavulana 62 huku wale wa daraja la nne wakiwa 179 na la kwanza hadi la tatu ni 27.
Shule ya Sekondari Mbande inao wanafunzi 117 wenye daraja sifuri wakiwamo wasichana 61 na wavulana 56, daraja la nne wamepata wanafunzi 270 na daraja la kwanza hadi la tatu wanafunzi 93.
Sekondari ya Juhudi Jeshini inayohitimisha shule saba zilizofanyiwa tathmini na gazeti hili, wanafunzi wake 170 wamepata daraja sifuri na 128 wakipata daraja la nne huku daraja la tatu hadi la kwanza likiwa na wanafunzi 37.
Mwananchi