Wachezaji Wazenji Watano waliobebwa na Kombe la Mapinduzi




MLANDEGE ya Zanzibar ilitwaa Kombe la Mapinduzi Ijumaa iliyopita baada ya kuichapa Singida Big Stars na kuhitimisha ukame wa miaka 13 kwa timu za hapo kutwaa ubingwa huo.

Mlandege ilipitia njia ngumu hadi kutwaa kombe hilo, ikiwa Kundi C ikiichapa Simba bao 1-0, na mechi ya nusu fainali ikaitoa Namungo kwa mkwaju 5-4 ya penalti, kabla ya kushinda mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali.

Hata hivyo, pamoja na kutotwaa ubingwa kwa miaka yote hiyo, lakini Kombe la Mapuduzi huwa kama jukwaa la wachezaji wa Kizanzibari kuonekana na klabu mbalimbali, hususan za Tanzania Bara.

Na msimu huu timu nyingi za Zenji zimefanya vizuri sana na wala haikuwashangza mashabiki wengi kuona moja ya timu za huko ikitwaa ubingwa. Kama kawaida ya miaka yote, baadhi ya wachezaji wameshaanza kuonekana na kuvutia klabu mbalimbali Bara.

Straika wa Mlandege, Bashima Sauli Saite, ameweka wazi kuwa ameshaanza kupokea simu kutoka Tanzania Bara zikihitaji huduma yake.


Straika huyo mwenye mwili uliojengeka kimichezo na aliyewasumbua sana mabeki wa Singida Big Stars, ameweka wazi kuwa kama si kipindi hiki cha dirisha dogo, basi msimu ujao ataonekana Bara.

Golikipa wa Mlandege, Yusuph Abdul Ally, aliyeonyesha uwezo mkubwa tangu kuanza kwa michuano hiyo na kuwa kipa bora wa mashindano, alisema mpira ni kazi yake, na tayari simu zimeshaanza kumiminika.

Katika makala haya tutawaangalia baadhi ya wachezaji waliowika kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kupata timu Bara, twende sasa...


#1. Ibrahim Rajab 'Jeba'

Mwaka 2012, kulikuwa na mchezaji aliyewika kwenye Kombe la Mapinduzi akiichezea Chuoni FC. Ni Abrahim Rajab 'Jeba.' Baada ya kumalizika kwa michuano hiyo alisajiliwa Tanzania Bara na Klabu ya Azam FC, licha ya kwamba Simba nayo ilikuwa ikimhitaji.

Simba ilitaka kuifanyia umafia Azam na kumsajili ilipomsajili mchezaji huyo na kujiunga nayo kwa mazoezi, lakini hakuweza kuichezea kwa kuwekewa ngumu na Azam FC iliyokuwa tayari na mkataba naye wa miaka miwili. Baadaye aliichezea pia Mtibwa Sugar kwa kipindi kirefu. Mchezaji hiyo alifariki dunia Zanzibar mwaka 2019.

#2. Feisal Salum 'Fei Toto'

Huyu ni mchezaji maarufu zaidi kwa sasa nchini. Fei Toto kabla ya kuvuka maji na kutinga Bara alikuwa akiichezea JKU ya Zanzibar. Baada ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka 2018, Klabu ya Singida United ilimsajili kwa mkataba wa miaka miwili.

Lakini kabla hajaanza kuitumikia, kiungo huyo mshambuliaji anayeichezea Zanzibar Heroes na Timu ya Taifa ya Tanzania, alipelekwa klabu ya Yanga ambayo yupo hadi leo, ingawa kwa sasa ana mgogoro wa kimkataba na klabu yake hiyo.


#3. Ibrahim Hilika

Mchezaji huyu amejiunga na Polisi Tanzania kipindi hiki cha dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar. Ibrahim Hilika, mtoto wa mchezaji wa zamani wa Zanzibar, Hamad Hilika, naye alionekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2018 na akawa mfungazaji bora akiwa na timu ya Zimamoto.

Msimu uliofuata Mtibwa wakaenda kumsajili baada ya kuona amekuwa na mwendelezo kutokana na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar 2019/20, hivyo Agosti 2020 akasajiliwa na klabu hiyo kabla ya kuihama kipindi hiki cha dirisha dogo.

#4. Hussein Abel Thomas

Ni mmoja wa magolikipa hodari kwa sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Alisajiliwa na Prisons kipindi cha dirisha dogo la usajili msimu uliopita.

Prisons ilimnyakuwa baada ya kuonyesha kazi nzuri na kushangaza wengi kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka jana akiwa na kikosi cha Taifa Jang'ombe na hadi leo si tu kipa namba moja, bali Thomas Abel ni mmoja wa makipa ambao wanatajwa huenda msimu ujao asiichezea tena Prisons kutokana na kiwango chake kikubwa, kwani klabu kadhaa zimeshaanza kummezea mate.


#5. Ibrahim Abdallah 'Bacca'

Pamoja na kutolewa kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka jana, Yanga haikurudi bara hivi hivi. Iliondoka na beki aliyefanya vizuri kwenye michuano hiyo akiwa na kikosi cha KMKM, Abdallah Hamad 'Bacca.'

Mchezaji huyo alipigiwa upatu mno na Nadir Haroub 'Cannavaro', ambaye naye ni mchezaji kutoka Zenji na aliichezea pia Yanga.

'Bacca' ambaye ni beki wa kati, bado yupo Yanga akiwa ni chaguo la pili kwenye kikosi hicho chini ya kocha Nasreddine Nabi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad