Yanga yamlipa Fei Toto mamilioni, mwenyewe auchuna



KAMA ulikuwa unadhani sakata la kiungo fundi wa mpira, Feisal Salum 'Fei Toto' na klabu ya Yanga limeisha, basi ngoma ndio kwanza bado mbichi baada ya timu hiyo kumwandikia barua ya kumtaka arudi kazi fasta.
Fei alitangaza kuvunja mkataba na Yanga aliyojiunga nayo mwaka 2018 kwa kulipa Sh 112 Milioni zikiwamo fedha za kuvunjia mkataba na mishahara wa miezi mitatu ambazo zilirejeshwa na klabu kabla ya kukimbilia Shirikisho la Soka (TFF) kumshtaki katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji.

Kamati ilitoa hukumu yake kwa kutamka kwamba Fei Toto ni bado ni mchezaji wa Yanga, huku kiungo huyo na watu wanaomsimamia wakishikilia msimamo kwamba alishajiondoa kikosini na kuendelea na mambo yake.
Mabosi ya Yanga wamendeleaa kumuwekea mshahara kwenye akaunti yake kama mtego flani kwake licha ya kutoonekana kazini na juzi iliamua kumlima barua ya kumtaka aende kazini haraka.

Yanga kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine imemuandikia barua rasmi Fei Toto akimtaka kurudi kazini kuendelea na majukumu yake lakini pia sakata la mkataba wake akiwa kazini.
Tayari inadaiwa barua hiyo imeshapokelewa na Fei Toto ambapo yeye na menejimenti yake nao wana hesabu zao, japo bado hawajaijibu barua ya Yanga kama atarejea kazini au vinginevyo.

Mbali na kumlima barua hiyo, lakini klabu hiyo imeendelea kumuingizia fedha kiungo huyo kama malipo ya mshahara wake na marupurupu, ikiwa ni mtego, huku upande wa mchezaji huyo ukiuchuna na kushikilia msimamo wa kujiondoa mazima klabuni na sasa inaelezwa wanajipanga kukata rufaa kupinga hukumu ya Kamati ya TFF.

Mwanaspoti linafahamu upande wa menejimenti ya Fei Toto, inapiga hesabu za kuomba marejeo ya uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyohukumu kwamba mchezaji huyo ni mali ya Yanga kwa mujibu wa mkataba wake.

Lengo la kutaka marejeo hayo ni kutaka kesi isikilizwe upya kisha ikishindikana kutolewa maamuzi mengine wakimbilie Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), huku ikielezwa kitendo cha Yanga kumuingizia Fei fedha za mshahara na stahiki zake ni kujiweka salama kisheria.

Mwananchi limedokezwa kuwa, Yanga imeshamlipa Fei Toto mishahara miwili ikiwa ni tafsiri kwamba wameendelea kumtambua kiungo huyo kama muajiriwa wake ndani ya klabu hiyo.

"Sisi tunaendelea kumlipa, utaachaje kumlipa mchezaji wako? Tunaheshimu taratibu za ajira, sasa barua tuliyomuandikia maana yake tunamtaka arejee kazini na akija kama atakuwa na malalamiko yoyote tutamsikiliza na kuangalia hoja zake lakini hayo yatafanyika akiwa anatokea kazini kwenye kituo chake cha kazi," alisema mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga.

Upande wa Fei haukupatikana, lakini taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa kiungo zinasema tayari ameongeza mwanasheria mwingine wa kuliongezea nguvu jopo lililopo linaloongozwa na wanasheria waliomsimamia Bernard Morrison katika sakata lake dhidi ya Yanga na kushinda.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad