Mwanaume anayesemekana kuwa na umri wa miaka 20, amefariki dunia baada ya kuanguka kutoka kwa mwamba wa Kit Mikayi eneo la Seme,kaunti ya Kisumu Kenya.
Mwanamume alifariki baada ya kuanguka kutoka kwa mwamba wa Kit Mikayi eneo la Seme, kaunti ya Kisumu.
Katika tukio hilo la Jumapili, Februari 19, mwendo wa saa nane asubuhi, marehemu alikuwa ameandamana pamoja na waumini wengine juu ya mwamba huo kuomba.
Lakini mambo yaligeuka baada ya mwanaume huyo kuteleza kutoka kwenye mwamba huo, ambao hutumika kama mahali pa maombi na kuanguka hadi kufariki, msimamizi wa eneo la Othany, Absalom Oyoo alithibitisha.
"Hakuna kitambulisho cha kumtambua marehemu ni nani na uchunguzi unaendelea," alisema Oyoo, kama alivyonukuliwa na Capital.
Msimamizi huyo alisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini namna marehemu alivyoanguka. Alitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Kisumu kulizungushia uzio kwenye mwamba huo ili kuzuia watu kuingia na kutoka bila kujulikana.
"Ingekuwa rahisi kuwafuatilia watu waliokuwa na marehemu kama walikuwa wametia sahihi kitabu cha wageni,” alisema.
Shughuli zozote za maombi katika mwamba huo zimesitishwa ili kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo chake.