Kibaha. Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam limeweka msimamo kuhusu utoaji huduma za kiroho kwa waumini wake, ambapo kuanzia sasa watakaohudumiwa ni wale wanaoshiriki ibada za jumuiya na kanisani.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Februari 11, 2023 wakati wa kikao cha Achidikonary ya Kibaha kilichofanyika mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Huduma hizo ni pamoja na mazishi, ndoa kipaimara, ubatizo na hata maombi mbalimbali yanayoendana na imani ya dhehebu hilo.
"Baba Askofu ameshasisitiza kuhusu hilo hivyo kuanzia sasa sisi wachungaji hatutahusika kutoa huduma hizo kwa waumini ambao watakiuka kanuni hizo," amesema Rogers Mshuza.
Mshuza ambaye ni Mchungaji kutoka Kanisa la Anglikana, Sofu Kibaha mkoani Pwani amesema kuwa hivi sasa baadhi ya waumini wamekuwa wakiyumba, leo yuko huku kesho yuko kule jambo ambalo linaweza kuleta mvutano hata kwa viongozi wa madhehebu mengine.
Kwa upande wake Kasisi kiongozi Kanisa Anglikana Kibaha, Exavia Mpambichile amesema kuwa utaratibu huo utasimamiwa na viongozi wa jumuiya kwani ndio wanaowatambua waumini wao.
"Sisi tutakuwa tunapokea taarifa kutoka kwa viongozi wa jumuiya ndio watakuwa wanatuletea ukweli pindi muumini anapofika kutaka kupata huduma yoyote ya kiroho kama ayasema hamtambui basi hatutahusika kwa lolote," amesema.
Amesema kuwa mipango iliyopo kwa sasa mbali na waumimi kusali pia wanaweka mikakati ya kuwepo miradi ya kiuchumi Ili kuwasaidia waumini.
Kwa upande wake, Hilaly Sagawala ameuomba uongozi wa Achidikonary hiyo kuwekeza elimu ya masuala ya kiuchumi kwa waumini wa Kanisa hilo ili waweze kutumia rasilimali mbalimbali kujikwamua kiuchumi.