BEKI wa kushoto wa Yanga Mkongomani, Joyce Lomalisa Mutambala ameahidi kuipambania timu yake kwa kucheza kwa kujitoa kwa ajili ya kupata ushindi katika mchezo huo.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni saa chache mara baada ya kupanda ndege kuelekea nchini Tunisia wakipitia Dubai kwa ajili ya mchezo wa hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga Jumapili hii saa moja kamili usiku wanatarajiwa kujitupa uwanjani kuvaana dhidi ya US Monastir ya Tunisia katika mchezo wao wa kwanza wa michuano hiyo.
Akizungumza na Spoti Xtra, Lomalisa alisema hautakuwa mchezo kwao mwepesi dhidi ya US Monastir ambao wenyewe watakuwa wenyeji wakiwa na sapoti kubwa ya mashabiki.
Lomalisa alisema kuwa lakini hiyo haimfanyi yeye pamoja na wenzake kuingia hofu, na badala yake watahakikisha wanacheza kwa nidhamu kubwa kufanikisha malengo yao ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Aliongeza kuwa kikubwa mashabiki wa Yanga wawape maombi watakapokuwepo uwanjani ili wapate ushindi wa kwanza wa ugenini utakaowaongezea hali ya kujiamini na kushinda mwingine unaofuatia dhidi ya TP Mazembe nyumbani.
“Niwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa, binafsi nitacheza kwa kujitoa na kuipa ushindi timu yangu ya katika mchezo huu wa kwanza shirikisho tutakapokuwepo ugenini.
“Uzuri binafsi pamoja na wachezaji wenzangu baadhi tuna uzoefu mkubwa wa michuano hii mikubwa, hivyo ni muda wa kuutumia kupata ushindi wa ugenini kabla ya kurejea nyumbani.
“Ninafahamu presha inakuwepo kubwa ugenini kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani, lakini kwa uzoefu wetu tutaachana na kelele zao na badala yake tutatimiza majukumu yetu ya uwanjani,” alisema Lomalisa.