Chadema Wanapaswa Kupata Umiliki wa Gari Alilopigwa Nalo Risasi Tundu Lissu Pamoja na Nguo zake Zenye Damu



TUNDU Lissu, alipigwa risasi 38. Kati ya hizo, 16 zilizama mwilini. Ni tukio la Septemba 7, 2017.


Tukio la Lissu ni kielelezo cha mapambano ya kisiasa nyakati za giza. Chuki za kisiasa zilifika mahali utu wa Mtanzania ulipotea.


Hivi karibuni Lissu alikwenda polisi, Dodoma, akataka kuona gari lake, aone kama anaweza kulitumia au alipeleke makumbusho. Wazo la kwanza, kulitumia, sio zuri, la pili ni sawa.


Katika wazo la pili, nina ushauri kwa Chadema. Ni kuhakikisha wanakuwa kitovu cha historia ya mashambulizi aliyofanyiwa Lissu.


Lissu alishambiliwa akiwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, mbunge wa chama hicho na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alifanya kila jitihada ndani ya uwezo kuhakikisha Lissu anavuta oksijeni leo. Mengine ni majaala ya Mungu.


Hivyo, Chadema hawatakiwi kuruhusu kutengwa na tukio la Lissu. Na kwa kuanza wanapaswa kumshawishi Lissu awauzie gari alilokuwa amepanda kipindi anashambuliwa.


Niliona hivi karibuni, Lissu alipofanya ziara nyumbani kwao, Ikungi, Singida, akakabidhi nguo alizokuwa amevaa siku ya shambulio kwa wazee. Swali, wazee wanapewa nguo ili iweje? Wafanye tambiko?


Chadema wanatakiwa wapate umiliki wa zile nguo. Gari, matundu yake, nguo hizo na damu zake, viwekwe makumbusho ya chama, vitumike kama sehemu ya kielelezo cha safari ya mapambano ya kudai demokrasia nchini.


Kama nguo alizovaa siku ya mwisho, alipopigwa risasi, Abraham Lincoln, Aprili 15, 1865, zipo hadi leo, takriban miaka 158 iliyopita, inashindikana nini nguo za Lissu kutunzwa, ziwe kumbukumbu ya chama?


Ukifika The Henry Ford, Detroit, Michigan, utakuta gari ambalo John Kennedy, alikuwa amepanda siku alipopigwa risasi, Novemba 22, 1963, Dallas, Texas. Haishindikani Chadema kuwa na makumbusho yao.


Umuhimu wa Chadema kumiliki kumbukumbu za tukio la Lissu ni kwa sababu yajayo ni mengi. Lissu anaweza kuhama chama, akastaafu siasa, isisahaulike, yeye ni binadamu. Chadema wanatakiwa kuhakikisha tukio la Lissu ni sehemu ya historia ya chama siku zote, si kwa nadharia, bali kwa mifano hai. Gari la Lissu na nguo zake ni mfano mkubwa.


Ndimi Luqman MALOTO

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad