DPP amfutia mashtaka Zumaridi, apewa masharti



Mwanza. Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) amesema hana nia ya kuendelea na shauri la jinai namba 11/2022 lililokuwa linamkabi Diana Bundala maarufu 'Mfalme Zumaridi' lenye shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu huku akiomba shauri hilo kuondolewa katika mahakama ya Mkoa wa Mwanza.

Shauri hilo lilikuwa limepangwa leo Jumatano Februari 8, 2023 kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi juu ya shauri hilo ili kwenda Mahakama Kuu kusikilizwa ushahidi wake Februari 9, mwaka huu lilisikilizwa kwa dharura katika chemba ndogo na Hakimu Mkazi mwandamizi wa mkoa huo, Boniventure Lema.

Akisoma maamuzi hayo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dorcas Akyoo amesema ofisi hiyo ya DPP imefikia uamuzi huo kufuatia kifungu cha Sheria Mwenendo wa Mashahidi namba 90 kifungu kidogo namba 11 Sura namba 20 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Akitangaza uamuzi wa kumuachia huru Zumaridi bila uwepo wa mawakili wake, Hakimu, Boniventure Lema amesema; "Sasa upo uhuru katika kesi hii namba 11/2022 hivyo unaweza kuendelea na shughuli zako lakini hii haitoathiri shauri lilokuweka hatiani."


Awali, Wakili Akyoo aliiomba mahakama hiyo kupokea maombi ya serikali ya kutaka mshtakiwa huyo (Zumaridi) awe chini ya uangalizi kwa kipindi cha miaka mitatu, asijihusishe na masuala yoyote ya uvunjifu wa sheria na amani katika maeneo yake sambamba na kuripoti ofisi ya upelelezi ya mMkoa wa Mwanza mara moja kwa mwezi.

Amesema maombi hayo yametolewa chini ya kifungu cha Sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai namba 70 na 72 (e) pamoja na kifungu namba 74 na 370 (a) cha sura namba 20.

Ili kufanikisha hilo, Akyoo alimtaka Zumaridi kuweka saini kwenye hati na kukubali maombi hayo mbele ya mahakama na kuahidi atakuwa mwenye tabia nzuri, atatunza amani na hatosababisha fujo yoyote kwa kipindi cha miaka mitatu.


Ilipofika Saa 8:23 mchana, Hakimu Boniventure Lema aliahirisha shauri hilo kwa dakika 30, kwa lengo la kutoa fursa kwa Zumaridi kutafakari na kutoa uamuzi, kama anakubaliana na mapendekezo hayo ya serikali bila uwepo wa mawakili wake, kutokana na shauri hilo kuitwa mahakamani hapo kwa dharura.

Baada ya kurejea, Wakili wa utetezi, Erick Muta aliyepewa taarifa ya shauri hilo kuitwa kwa dharura mahakamanihapo, aliwasili na kukubali baadhi ya maombi yaliyotolewa kwa njia ya mdomo huku akieleza maombi mengine yanaondoa haki ya msingi ya kikatiba ya mteja wake huru.

Alisema hiyo ni kutokana na maombi hayo kujengwa katika msingi wa mashaka na hofu ya kumnyima mpokea maombi kuwa huru, pindi akiwa uraiani.

Baada ya hoja hiyo, wakili Akyoo akasema lengo la kufikisha ombi hilo ni kwa ajili ya kumfanya mjibu maombi (Zumaridi) asijihusishe na vitendo ambavyo awali alishtakiwa navyo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lema aliahirisha utolewaji wa majibu hadi Februari 14, mwaka huu Saa 3 asubuhi.

Baada ya uamuzi huo, Zumaridi ambaye alihukumiwa kutumikia kifungo katika kesi namba 10/2022, alirejea gerezani kumalizia siku 10 zilizosalia katika kifungo hichoi kwani tayari ameshatumia siku 20.

Zumaridi alihukumiwa kwenda jela kwa kosa la kuwazuia maofisa wa umma kutekeleza wajibu wao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad