SIMULIZI ya washambuliaji wawili kutoka Congo ambao walifika Tanzania kuichezea klabu ya Yanga. Inanikumbusha namna gani mpira wetu ulikotoka na ulipo na pengine uendako.
Ni takribani miaka 30 sasa tangu staa wa zamani wa kimataifa wa Congo, Nonda Shaaban ‘Papy’ alipokuja nchini akitokea Burundi. Alitua akacheza Yanga iliyokuwa na washambuliaji wawili wakali. Aliwakuta Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ pamoja na James Tungaraza tuliyemzoea kumuita kwa jina la ‘Boli Zozo’.
Nonda alikuwa mkali lakini akajikuta anasugua benchi mbele ya Mmachinga na Boli Zozo. Bahati yake akapangwa mechi fulani ya kimataifa akaonekana na klabu ya Vaal Professional ya Afrika Kusini. Hii ndio ilikuwa njia yake ya kutokea.
Kuanzia hapo akaenda zake kucheza FC Zurich ya Uswisi. Akaenda Ufaransa. Akaenda Uingereza. Akawa mchezaji mwenye jina kubwa duniani kuliko wale waliokuwa wanamuweka benchi pale Yanga. Imenipa maswali mengi.
Moja kati ya sababu iliyomfanya Nonda aondoke kwa urahisi nchini ni kwamba hakuwa mchezaji tegemeo. Kama angekuwa tegemeo nadhani kuna mtu angechapwa viboko kwa kumruhusu Nonda kuondoka nchini. Ni tamaduni zetu kuzuia wachezaji wazuri kuondoka, hasa kwa wakati huo.
Leo Yanga wana mshambuliaji hatari wa Congo anayeitwa Fiston Mayele. Pale mbele hakuna mshambuliaji yeyote anayeweza kumuweka benchi. Najaribu kujiuliza kama Mayele angekutana na Mmachinga na Boli Zozo, je angetamba? Au angedoda kama Nonda?
Hii imenipa tafakuri pia ya kwanini mpaka leo rekodi ya Mmachinga inaendelea kuwasumbua washambuliaji wetu wa sasa. Kuna msimu alifunga mabao 26 peke yake. ni rekodi ambayo wanahangaika nayo mpaka sasa.
Kumbe Mmachinga hakufunga mabao hayo kwa bahati mbaya. Kumbe alikuwa mkali. Kitendo cha kumuweka Nonda benchi kilithibitishwa na mabao ambayo alifunga kwa wakati huo. Lakini hapo hapo inanikumbusha namna gani ambalo taifa letu limekuwa na uzembe kwa muda mrefu.
Kumbe si ajabu Mmachinga na Boli Zozo kama wangeondoka wakafuatana na Nonda katika safari yake si ajabu leo wangekuwa majina makubwa duniani. Nchi yetu huwa inakatisha tamaa kila unapofikiria namna gani tulianza kupoteza nafasi adimu tangu enzi za zamani huku wenzetu wakizitumia vema.
Lakini hapo hapo tujaribu kujiuliza. Leo anayetamba pale mbele ni Mcongo. Kama wakati huo Mcongo ambaye alikuwa anasota benchi alifanikiwa kwenda nje na kutamba vile leo akija wakala kuitazama Yanga? Nadhani bado ataondoka na Mcongo mwingine.
Wakati ule akina Mmachinga waliziringia tu nafasi za kucheza nje lakini leo kama Mayele mwenyewe hachezi Ulaya unadhani ni mchezaji gani mzawa pale mbele katika safu ya Yanga anaweza kucheza Ulaya? Sidhani.
Hata katika soko la ndani ya Afrika kwa sasa wachezaji walioondoka hivi karibuni walikuwa wageni. Clatous Chotta Chama, Tuisila Kisinda na Jose Luis Miquissone wote hawa ni wageni. Hakuna Mzawa aliyeuzwa katika siku za karibuni. Wa mwisho kuuzwa alikuwa Simon Msuva.
Jaribu kuangalia mawinga wazawa waliokwenda Yanga baada ya yeye kuondoka. Wote wapo chini yake. kuanzia Juma Mahadhi, Dennis Nkane hadi Dickson Ambundo. Wote hawamfikii Msuva. Inamaanisha kila siku tunakwenda chini.
Kuanzia Nonda kuwekwa benchi hadi leo Mayele kutamba pale mbele inakuthibitishia ni namna gani vipaji vya wazawa vimeanza kudidimia kwa muda mrefu sasa. Inakupa tu tafukuri nyingine kwamba huenda Mayele kama angewakuta Mmachinga na Boli Zozo basi angekuwa mshambuliaji wa akiba Yanga.
Ukiachana na hao, unaweza tu kuangalia katika nafasi nyingine. Joyce Lomalisa asingeweza kucheza nafasi ya Ken Mkapa. Yannick Bangala asingeweza kucheza nafasi ya Method Mogella. Lakini pia Jesus Moloko hafiki hata robo ya Edibily Lunyamila.
Tunafanyaje kurudisha vipaji hivi? Sijui. Ninachofahamu ni kwamba sioni kama tunaweza kurudi tulikotoka. Sioni kama tunaelekea kupata wachezaji wa kumuweka benchi Mayele kama Mmachinga na Boli Zozo walivyofanya.
Huwa naongea na watu wa Simba, Yanga na Azam. Wananiambia kwamba sio kwamba wanakwenda kusaka mastaa nje kwa ajili ya fasheni. Hapana. Ni kwa sababu vipaji wanavyovisaka hawavioni nchini. Hauwezi kuwakatalia.
Katika mechi za kimataifa hapa majuzi Simba walikuwa wanatamba. Ukiangalia sababu za kutamba kwao ni wageni akina Chama, Miquissone, Meddie Kagere, Paschal Wawa na wengineo. Kama ungeipanga Simba yenye wazawa watupu sidhani kama tungefika katika hatua ya makundi.
Hapo hapo unaweza kupima kwa Yanga ambayo ilifika hatua ya robo fainali Ligi ya mabingwa mwaka 1998. Wachezaji wote walikuwa wazawa.
Simba walioitupa nje Zamalek pale Cairo Misri ilikuwa na mgeni mmoja tu, Ramadhan Wasso. Leo sioni timu hizi zikitoboa kwa kutumia wachezaji wa ndani tupu.
Nimewatafakari Nonda na Mayele nimegundua kwamba wanatoa ishara ya kushuka kwa soka letu. Kuanzia wakati huo mpaka sasa tunadumaa kwenda chini. Mwache Mayele atambe.
Amekuja katika nyakati ambazo labda atapata upinzani kutoka kwa mshambuliaji kutoka nje. Sioni akipata upinzani kutoka kwa washambuliaji wa ndani.