KATIKA mechi ya mwisho ya kundi lao Simba inaweza isipite halafu watakumbuka pambano lao la kwanza la kundi C katika michuano hii na kutikisa vichwa kwa masikitiko. Simba ilipoteza kwa bao moja dhidi ya Horoya ya Guinea.
Wataondoka Conakry kwa masikitiko makubwa, lakini bila ya kusahau kumshukuru kipa wao, Aishi Manula aliyecheza penalti ya kipindi cha pili. Huenda wangepoteza kwa mabao mawili kama sio juhudi za Manula. Hata hivyo hii sio mara yake ya kwanza. Kumfunga Manula penalti kunahitajika utulivu mkubwa.
Masikitiko yao makubwa yatakuwa kwa John Bocco aliyepoteza nafasi tatu, huku moja ikiwa ya wazi zaidi baada ya kuwatambuka walinzi wa Horoya, lakini akashindwa kumchambua vyema kipa wao na kujikuta akiupeleka mpira nje. Simba wangeondoka na pointi moja pale Guinea ingewasaidia.
Na sasa wana kazi kubwa wikiendi ijayo. Wanacheza na Raja Casablanca pale Temeke. Simba watalazimika kuwa katika ubora wao wa kila kitu kukabiliana na Raja. Lakini zaidi watalazimika kurudia enzi zao za kuufanya uwanja wa Mkapa kuua wapinzani wao. Iliwahi kutokea miaka ya karibuni tulipoambiwa kwamba ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’.
Ndani na nje ya uwanja Simba wanahitaji kuwa katika ubora wao. Ndani ya uwanja ubora ule wa kina Clatous Chama, Luis Miquissone, Rally Bwalya, Sergie Wawa na wengineo. Wakati ule kuna wakubwa walikufa kwa Mkapa katika namna ambayo isingeelezeka kirahisi. Ndani ya uwanja tulikuwa tunaona kinachofanyika, nje ya uwanja mashabiki walitimiza wajibu wao lakini hata viongozi walitimiza wajibu wao.
Nahofia ubora wa Raja Casablanca. Siku moja kabla Simba hawajafungwa Conakry, Vipers ya Uganda ilikuwa inachanwa kama karatasi dhidi ya wembe pale Casablanca. Kwa waliotazama ile mechi imetia hofu kwa kiasi kikubwa. Itawezekana vipi kila kitu kubadilika ndani ya wiki moja tu?
Inawezekana vipi Simba kushusha kiwango cha Raja ndani ya wiki moja? Hii mechi imekaa kimtego. Simba wanahitaji pointi tatu za lazima. Katika hatua ya makundi ya michuano yoyote yenye timu tatu inakuwa ngumu kuvuka kama ndani ya mechi mbili unaambulia pointi moja tu. Hii namaanisha kama Simba wakienda sare na Raja wikiendi ijayo.
Ukweli ni kwamba hata sare itakuwa ngumu kama Raja wataachiwa wacheze kama walivyocheza dhidi ya Vipers. Lakini Simba ndivyo ilivyo. Inaweza kubadili kibao. Inaweza kushusha kiwango cha mpinzani ndani ya wiki moja tu na kisha tukajikuta tukiwashangaa wapinzani katika uwanja wa Mkapa.
Al Ahly waliwahi kuwa na kiwango bora katika mechi za klabu bingwa ya dunia ambapo walicheza na Bayern Munich katika fainali wakapoteza kishujaa lakini ndani ya siku 10 baadaye wakafungwa kizembe na Simba katika uwanja wa
Mkapa. Kinachonitia hofu ni kwamba ilikuwa Simba tofauti kidogo na hii. Nahisi hii hapa makali yamepungua. Kibu Dennis sio Miquissone.
Hata hivyo vyovyote ilivyo Simba wanahitaji pointi tatu. Kama wakizikosa hizi pointi tatu wanaweza kutupwa nje ya kundi kwa urahisi tu. Hapa katikati wanaweza kurukaruka lakini isije kutokea kwamba pambano lao la mwisho liwe na umuhimu mkubwa. Ni kwa sababu watakuwa wanacheza na Raja ugenini. Waarabu hawapendi kupoteza mechi kwao hata kama wameshafuzu katika kundi.
Mambo mengi yanatia hofu katika mechi ya wikiendi hii. Simba wameungana kweli baada ya tukio la uchaguzi kupita. Simba huwa wanakuwa wamoja sana kuelekea katika mechi kama hizi. Hata hivyo pambano hilo halijaja katika wakati mzuri. Uchaguzi uliopita umewaacha baadhi ya vigogo wa Simba wakiwa vipande vipande.
Nahofia wasije kutumia mechi hizi kuombea timu ifungwe ili walete zile kauli zao “tuliwaambia hao watu hawawezi kuwafikisha popote”. Mara nyingi kuna roho zinaombea timu ipoteze ili kujaribu kuthibisha umuhimu wao ndani ya klabu. Nazifahamu klabu kubwa. Zina watu wa tabia hii ambao wapo tayari kuona hata timu ikipoteza kwa ajili ya kulinda maslahi yao.
Lakini ni wazi pia kwamba Raja watataka kumaliza kazi yao Uwanja wa Mkapa. Wakipata pointi sita ndani ya mechi za kwanza huku mechi ya tatu wakirudi nyumbani wanaweza kujikuta wakivuka hatua hii ndani ya mechi tatu tu za awali. Mara nyingi Waarabu wanapenda jambo hili. Lakini hata pointi nne ndani ya mechi mbili kwao sio jambo la ajabu kwa sababu wana uhakika wa kushinda mechi mbili zilizobaki nyumbani na kutimiza pointi 10.
Ndani ya uwanja mchezaji ambaye atatazamwa sana ni Patrick Phiri. Ndani ya wiki moja Simba watakuwa hawana imani na Bocco na ndivyo tulivyo. Najua kocha Robertinho atapigwa presha kumuweka nje Bocco baada ya kupoteza nafasi zake alizopata pale Guinea.
Mshambuliaji yeyote ambaye atapangwa basi mashabiki watatazamia mambo makubwa kutoka kwake. Wakati ule Simba ikifanya vyema katika michuano ya kimataifa iliwategemea zaidi Meddie Kagere, Bocco na Chris Mugalu. Sasa hivi mashabiki watakuwa wanamtegemea zaidi Phiri.
Lakini hapo hapo Chama na Saido Ntibanzokonza inabidi wakifanye kile ambacho Chama na Miquissone waliwahi kukifanya katika michuano mikubwa kama hii katika siku za awali. Wasipofanya hivyo maisha yatakuwa magumu kwa Simba katika michuano hii. Wachezaji wakubwa wanaibeba timu katika mechi kubwa.
Vyovyote ilivyo Simba hawajaanza salama katika michuano hii. Endapo Horoya atamfunga Vipers basi maisha yatakuwa magumu zaidi kwa Simba. Kinachotakiwa ni kwa Vippers kumfunga Horoya ili timu nyingine ya pili isiende mbali katika msimamo kwa sababu ni wazi Raja wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kupita kundi lenyewe.
Sioni kama Vipers wanaweza kumzuia Raja katika pambano jingine la marudiano katika uwanja wowote wa soka Afrika. Lakini hata nilivyowaona Horoya sioni kama wanaweza kumzuia Raja katika mechi mbili za soka. Labda maajabu yatokee. Raja wanaonekana kujiandaa haswa.