Juma Mgunda "Tumeisoma Timu Horoya AC Ligi ya Mabingwa Barani Afrika



Kocha Msaidizi wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema kikosi chao kinaendelea kujiandaa na mchezo wao wa kwanza wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC.


Simba SC itacheza ugenini Jumamosi (Februari 11), katika Uwanja wa General Lansana Conté, mjini Conakry, huku ikiwa na kibarua cha kuvunja Rekodi yake ya kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo.


Kocha Mgunda amesema tayari wameshaifuatilia Horoya AC na wametambua uzuri na udhaifu wa kikosi chao, hivyo wanachokifanya kwa sasa ni kujikita kwenye mbinu watakazozitumia kwenye mchezo huo wa Jumamosi.



Hata hivyo Kocha huyo mzawa amesema, wanakwenda Guinea wakiwa na tahadhari kubwa, huku wakitambua umuhimu wa mchezo huo ambao utaanza mishale ya saa kumi jioni kwa saa za Tanzania.


“Tumeona ubora wa Horoya AC, wako vizuri, tunaenda Guinea kwa tahadhari kubwa, wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huo, ni kufuata alama moja ama zote tatu.”


“Tunaendelea kuimarisha kikosi chetu hususan safu ya ulinzi na ushambuliaji ambayo itakua na kila sababu ya kupambana ili tupate matokeo ugenini.”


“Wakati tukipambana kwenye mchezo huo, tunapaswa kutoruhusu wapinzani kupata bao, tunahitaji kuwa makini kutafuta alama hata moja katika mchezo huo wa ugenini, kabla ya kurejea nyumbani kwa ajili ya kutafuta alama tatu za nyumbani.” amesema Mgunda


Amesema malengo yao makuu ni kusaka alama tatu muhimu za kila mchezo watakaocheza Hatua ya Makundi, lakini nguvu kubwa wameiweka nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.


Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kesho Alhamis (Februari 09) alfajiri, kuelekea mjini Conakry-Guinea kupitia Adis Ababa-Ethiopia.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad