Kada wa NCCR-Mageuzi aokotwa msituni



Dar es Salaam. Ikiwa imepita wiki moja tangu kutoweka kwa kada wa NCCR-Mageuzi Nicolus Clinton, chama hicho kimesema ameokotwa juzi na wasamaria wema ndani ya msitu nje ya Mkoa wa Dar es Salaam akiwa na hali mbaya.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa Umma wa NCCR - Mageuzi, Edward Simbeye baada ya kupata taarifa na kulijulisha Jeshi la Polisi, liliwajibika na sasa Clinton anaendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea kuimarika.

Alisema chama hicho kinalaani kitendo alichofanyiwa Clinton kwa kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo, alikiri kuzipata na kuahidi kufanya uchunguzi, ikiwamo kumuhoji mhusika ili kujua ukweli wa tukio hilo.


“Ni kweli taarifa za kutoweka kwa kijana huyo tulizipata, na taarifa za kuokotwa tumezipata, niseme tu jukumu la Jeshi la Polisi ni kufanya uchunguzi, ikiwamo kumhoji mhusika,” alisema Muliro.

Kamanda Muliro alisema katika tukio la namna hiyo, uchunguzi huanzia kwa mhusika mwenyewe, hivyo taratibu za kumhoji zinaendelea, ukweli utakapobainika taarifa itatolewa.

Januari 24 mwaka huu, Clinton alidaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha saa nne usiku akiwa nyumbani kwake Buguruni Malapa, baada ya kumueleza rafiki yake kuwa anaenda kupunga upepo nje kwa kuwa ndani ni joto.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa baada ya muda rafiki yake alipitiwa na usingizi na aliposhtuka aligundua Clinton hajarudi, huku simu zake zikiwa kwenye chaji, ndipo alipotoa taarifa kwa ndugu pamoja na viongozi wake.

Juhudi za kumtafuta zilianza, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Buguruni na kufungua jalada la uchunguzi namba 469, kupiga simu kwa ndugu zake na mzazi mwenzake lakini hawakufanikiwa.

Hata hivyo, viongozi wa NCCR hawakutaka kuweka wazi jina la msitu alikookotwa Clinton wala hospitali aliyolazwa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad