Kampuni ya ndege ya Precision Air limesema ndege aina ya PW 600 imeshindwa kufika Uwanja wa Ndege wa Dodoma, na hivyo kurejea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, baada ya rubani kupokea taarifa kwenye mifumo ya uendeshaji hivyo kuchukua tahadhari kwa ajili ya ukaguzi zaidi.
Akizungumza na Swahili Times Afisa Masoko kutoka Precision Air, Hillary Mremi amethibitisha taarifa hiyo ambapo ameeleza kuwa kwa taratibu za kiusalama rubani akipata taarifa kwenye mifumo ya uendeshaji huchukua tahadhari kulingana na taratibu zilizowekwa.
“Katika hili alipata tahadhari katika mfumo wa injini na aliizima ili kuitunza injini. Taratibu zinaelekeza kutua kwenye kiwanja kilichopo karibu kwa ukaguzi zaidi. Na kwa wakati huo uwanja wa karibu bado ulikuwa ni Dar es salaam na si Dodoma kama inavyoripotiwa,” amesema.
Aidha, kampuni hiyo limeeleza kuwa ndege zote hufanyiwa matengenezo kwa mujibu wa taratibu za kiusalama nchini na kimataifa na zinakaguliwa mara kwa mara na mamlaka husika za ndani na kimataifa.