Dar/mikoani. Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya kuangalia namna ya kuboresha Haki Jinai ikianza kazi, umeibua mambo mazito, yakiwemo maombi ya kutaka Serikali kurejesha fedha na mali zilizotaifishwa kwa washtakiwa wa uhujumu uchumi.
Aidha, tume hiyo imetakiwa kuitisha kikao cha kuwasikiliza wananchi waliokumbana na kadhia mbalimbali za ukiukwaji wa haki na waliohusika katika matukio hayo wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika hilo, wadau wa haki jinai waliozungumza na gazeti hili jana walisema, kuna wananchi walikutana na kadhia za ukiukwaji wa haki za binadamu na kujikuta mali zao kama majumba, magari, viwanja, madini na fedha taslimu zikitaifishwa.
Wadau hao wameeleza hayo ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia azindue tume hiyo ya watu 11 inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman kupitia mifumo ya taasisi za utoaji haki.
Taasisi hizo ni Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mahakama na Jeshi la Magereza.
Nyingine ni Jeshi la Uhamiaji, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Rais Samia ameipa tume hiyo miezi minne kuanzia jana akisisitiza kuwa “mfumo wa haki jinai nchini umevurugika.”
Katika hilo, ndipo Rais akagusia malalamiko yanayoelekezwa kwenye Ofisi ya Taifa ya Mashtaka juu ya fedha zilizokusanywa kwa njia ya majadiliano na DPP na kuonyesha utata uliopo kuhusu kiasi kilichokusanywa na wapi zilipo fedha hizo.
“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kulikuwa na ngoma kubwa kidogo inachezwa, mpaka kukusanya fedha za wale wa plea bargaining. Pesa zile nyingine zinaonekana na nyingine hazionekani. Ukifuatilia unaambiwa kuna akaunti China, sijui zimepelekwa pesa zipi. Tukatizame haya yote, kuna nini hasa kilichoikumba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” alisema Rais Samia.
Isikilize wananchi kwa uwazi
Kufuatia hali hiyo, Wakili Jerome Msemwa alizungumza na Mwananchi jana akisema kuunda tume ni jambo zuri lililochelewa, lakini ina wajumbe wenye weledi mkubwa, hivyo wananchi wanatarajia itatoka na mambo yatakayosaidia kupata haki zao.
Wakili hiyo alipendekeza tume hiyo izungumze wazi suala la makubaliano baina ya DPP na washtakiwa, akisema ni shauku ya wengi kujua kilichotokea kwa kuwa ni moja ya vilio vyao.
“Nadhani tume ingeweza kuweka public hearing (kikao cha kuwasikiliza wananchi), yaani watu waje watoe maoni yao, waseme wote ambao walikuwa wameathirika, iwape nafasi walete ushahidi wao ili mambo yote hayo yajadiliwe na Serikali,” alisema Msemwa.
“Malalamiko ni makubwa na hata ukiangalia kwenye mitandao ya kijamiii, yamezungumzwa sana hayo mambo. Nadhani utekelezaji wake ulikuwa na mizengwe mingi na watu wengi hawakutendewa haki. Watu wakisema ndipo tutagundua uzuri na kasoro zake na kuzirekebisha,” alisema.
Mawazo ya wakili huyo hayako mbali na ya Onesmo ole Ngurumwa, mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) aliyemshauri Rais Samia kuunda Tume ya Ukweli na Upatanishi.
Alisema tume hiyo itaunganisha tume zote ili kuchunguza mambo yote yaliyofanyika katika utawala uliopita na kushauri hatua bora za kuchukua ili yasije kujirudia.
Ole Ngurumwa alisema kuna mengi yalitokea katika utawala uliopita na yanahitaji maridhiano kama Taifa kuliko kuwa na tume ndogondogo ambazo zimekuwa zikiundwa.
Hata hivyo, Mhadhiri mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Tumaini-Makumira, Dk Elifuraha Laltaika alisema ana imani kubwa na tume hiyo kwamba itafanya uchunguzi wa kina juu ya madhila yote ya ‘plea bargaining.’
“Rais ameipa uzito mkubwa tume ambayo ameunda. Wachunguze suala hili na mengine na ambao watapatikana na hatia waadhibiwe na matokeo ya tume yasiishie kwenye makabrasha,” alishauri.
Utaratibu wa majadiliano kati Ofisi ya Taifa ya Mashtaka au Wakili wa Serikali na washtakiwa ulianzishwa baada ya marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) yaliyofanywa na Bunge Septemba 2019 yakilenga kumwezesha mshtakiwa kukiri makosa na kutoa taarifa kusaidia kupatikana kwa ukweli wa makosa.
Amwandikia barua Rais
Wakati wasomi na wadau wa haki jinai wakisema hayo, mfanyabiashara Peter Zakaria amezungumza na gazeti akiweka bayana alivyoathirika na majadiliano hayo na mali zake na za mkewe zenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni kuchukuliwa ili awe huru mwaka 2019.
Alisema tayari amemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan kuomba kurejeshewa mali hizo na kuwa hadi jana hakuwa amejibiwa barua yake.
“Nimemwandikia barua Rais kuomba nirejeshewe nyumba na kituo changu cha mafuta vilivyoko jijini Mwanza; mali zote zina thamani ya zaidi ya Sh200 milioni,” alisema Zakaria
Mbali na hizo, Zakaria anadai kiwanja namba 242 Block T kilichopo Barabara ya Kenyatta jijini Mwanza kilichowahi kuwa mali ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza) kabla ya kuuzwa kwa mke wa Zacharia, Antonio Zakaria na mwenzake Timoty Kilumile.
Wawili hao baadaye walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, kesi iliyowaweka mahabusu kwa kipindi kirefu kabla ya kuachiwa baada ya kukiri kosa kutokana na majadiliano na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Baada ya kukiri kosa, washtakiwa hao walihukumiwa kulipa faini ya Sh54 milioni kiwanja hicho kikitaifishwa.