Kocha Matola Mjanja Ashtukia Jambo



KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola ni kama ameshtukia jambo baada ya kuamua kurudi darasani kusoma lugha ili kwenda sawa na makocha wakubwa wanaokuja kufundisha soka hapa nchini, hususan ndani ya klabu hiyo kongwe.

Matola bado yupo darasani akiwa anasomea ukocha kozi ya Leseni A ya Caf, ambapo kituo chake kipo Zanzibar, lakini kwa sasa yupo Dar es Salaam akisubiri kwenda tena mafunzoni baada ya mwezi mmoja na kujiongeza kwa kuongeza ujuzi kwenye lugha.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli na Polisi Tanzania, ameanza masomo ya Lugha ya Kiingereza, Kifaransa na pia akiongeza na somo la kompyuta kwenye chuo kimoja maarufu kinachosomwa na watu kadhaa maarufu hapa nchini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matola alikiri ameamua kwenda kusomea lugha na kompyuta kwa malengo ya kujiandaa na changamoto za maisha hapo mbele baada ya kumaliza kozi yake, kwani anafahamu ni mambo ambayo atatakiwa kuwa anayafahamu ili kurahisisha kazi yake.


Hata hivyo, pamoja na kukiri kuwa anafahamu vizuri Kiingereza, amesema kuna baadhi ya vitu anatakiwa kuongeza kichwani kwake ili aweze kwenda sawa na makocha wakubwa wanaokuja hapa nchini na wa nje ya nchi.

“Nipo shule nasoma, achana na ishu ya Leseni A, lakini nasoma pia Lugha za Kiingereza na Kifaransa wakati huohuo naongeza ujuzi kwenye kompyuta, malengo ni kwenda sawa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, unajua, baada ya kumaliza kozi malengo yangu yatakuwa ya juu sana, hivyo lazima nijiandae mapema,” alisema kiungo nyota huyo wa zamani wa kimataifa na kuongeza;

“Kifaransa nilikuwa sikifahamu, ila kwa sasa naanza kuelewa na siwezi kupata shida hata nikifundisha kwenye nchi wanayoongea lugha hiyo, lakini kiingereza naongeza baadhi ya mambo ambayo yatakuwa na manufaa kwangu kwenye kazi yangu.


“Hata kama hapo mbele nitafanya kazi na kocha ambaye anazungumza Kifaransa basi nitakuwa nimeshapunguza mzigo hili ni jambo ambalo nilikuwa nataka kusoma kwa muda mrefu sana, nikirudi darasani Zanzibar, nitasimama kwanza nikija Dar naendelea.”

Matola anasema kuna umuhimu mkubwa kwa makocha wa kisasa kujua lugha kwani inawasaidia kwenye mambo mengi hata kozi nyingi ambazo wanafundishwa zinakuwa za Lugha ya Kiingereza.

“Sasa hivi Tanzania tunasajili wachezaji wengi, wanatoka kwenye nchi zinazozungumza Kifaransa na Kiingereza ni jambo zuri kwa makocha nao kujua hizo lugha, lakini pia kompyuta kwa kuwa dunia sasa imebadilika na tunaishi kisasa zaidi sasa,” alisema Matola aliyewahi kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini katika klabu ya SuperSport.

Matola aliyewaji kukipiga Kagera Sugar hajaonekana kwenye benchi la Simba tangu Kocha Mbrazili, Roberto Oliviera Robertinho alipojiunga na timu hiyo na inaelezwa kuwa anaweza kujiunga na timu hiyo siku chache zijazo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad