KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi amesema kuwa hataki kurudia makosa makosa matatu waliyoyafanya dhidi ya US Monastir ya nchini Tunisia katika mchezo wao na TP Mazembe ya DR Congo.
Yanga katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Afrika, walifungwa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir ugenini na Jumapili hii wanatarajiwa kuwakaribisha TP Mazembe katika mchezo wao wa pili kwenye Dimba la Mkapa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatano, Nabi alisema kuwa mara baada ya mchezo alifanya kikao na wachezaji huko Tunisia na kuuchambua mchezo huo dhidi ya US Monastir na kikubwa kuangalia upungufu wao.
Nabi alisema kuwa, kitu cha kwanza ambacho anataka kukiona kwa wachezaji wake ni kucheza kwa nidhamu pia wasiruhusu mipira ya kutenga nje ya 18 kwani wapinzani wao ni wazuri wa mipira ya vichwa.
Alitaja jambo la pili ni kutoruhusu mipira ya krosi golini kwao, hivyo mabeki wa pembeni wana kibarua kigumu kuelekea mchezo huo.
Na jambo la tatu ni kushambulia kwa kushtukiza na kumiliki mpira muda wote bila ya kuwapa nafasi wapinzani wao.
“Kocha Nabi hakufurahishwa na matokeo dhidi ya US Monastir, hivyo amepanga kuwafurahisha mashabiki katika mchezo dhidi ya Mazembe kwa ushindi nyumbani.
“Hivyo mara baada ya mchezo huo, haraka alianza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Mazembe kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Nabi alishawaangalia Mazembe katika michezo yao mitatu ya mwisho ya ligi na kimataifa kuhakikisha anawadhibiti wachezaji hatari na wenye madhara,” alisema Nabi.
STORI NA WILBERT MOLANDI, SPOTI XTRA