Mama asimulia alivyojaribu kunyonya maziwa yake kuokoa maisha




Uturuki. Mama wa watoto wawili, Necla Camuz amesimulia madhila aliyopata akiwa chini ya kifusi na mtoto wake mchanga aliyemzaa Januari 27, 2023 baada ya kuporomoka ghorofa alilokuwa akiishi kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini humo  Jumatatu wiki iliyopita.

 Mama huyo alidondokewa na kifusi cha ghorofa Februari 6, 2023 baada ya tetemeko la ardhi lililozikumba nchi za Uturuki na Syria akiwa na mwanaye huyo, amesimulia baada ya njaa kali chini ya kifusi hicho ilifika hatua akajaribu kunyonya maziwa yake bila mafanikio.

Akizungumza na mtandao wa BBC Swahili, Februari 13, Mama huyo amesema ilikuwa saa 4:17 alfajiri, alikuwa macho akimlisha mwanaye Yagiz nyumbani kwao katika Mkoa wa Hatay, Kusini mwa Uturuki, kabla ya kujikuta wakiwa wamefunikwa na kifusi.

Necla amesema katika ghorofa hilo la pili walikuwa wakiishi na familia yake.


"Tetemeko la ardhi lilipoanza, nilitaka kwenda kwa mume wangu ambaye alikuwa katika chumba kingine, naye alitaka kufanya hivyo, lakini haikuwezekana.

"Lakini alipojaribu kuja kwangu na mtoto wetu mwingine, kabati la nguo liliwaangukia na haikuwezekana kutusogelea.

"Tetemeko lilipozidi kuwa kubwa, ukuta ulianguka, chumba kilikuwa kinatikisika, na jengo lilikuwa linaporomoka. Tetemeko lilipotulia, sikugundua kuwa nilikuwa nimeanguka ghorofa moja chini. Nilipiga kelele kuita majina yao lakini hakukua na mawasiliano tena," amesema.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 33, amesema alijikuta akilala chini na mtoto wake akiwa amekumkumbatia kifuani. Amesema kabati lililoanguka karibu naye lilikuwa limeokoa maisha yao kwa namna moja au nyingine kwa kuzuia vipande vya matofali kuwaangukia.

Anasema akiwa amevaa nguo zake za kulalia chini ya kifusi, hakuona chochote kutokana na giza, kwa hiyo ilimbidi atumie hisia kutambua kilichokuwa kikiendelea.

Kwa bahati, anasema aliweza kubaini kwamba mtoto wake Yagiz alikuwa bado anapumua.

Amesema kwa sababu ya vumbi pamoja na joto kali, mwanzoni yeye pamoja na mtoto wake walipumua kwa tabu, lakini baadaye kadiri muda ulivyosogea walimudu hali hiyo.


“Zaidi ya kabati la nguo, mtoto wake mchanga, na nguo walizovaa, hakuweza kuona chochote isipokuwa kugusa vipande vya matofali na uchafu,” amesema.

Amesema muda ulipokuwa ukisogea zaidi alisikia sauti na hivyo alijaribu kupiga kelele kuomba msaada na kugonga kabati.

"Kuna mtu huko? Kuna mtu anaweza kunisikia?" aliita kwa sauti, lakini hakuna aliyejibu.

Amesema kutokana na hali ya giza kwenye kifusi, alianza kukata tamaa.


"Unapanga mambo mengi baada ya kupata mtoto, halafu ghafla unajikuta kwenye kifusi," amesema.

Hata hivyo, anasema alijua kwamba alipaswa kumtunza Yagiz na aliweza kumnyonyesha katika mazingira hayo magumu.

Anaeleza kutokana na njaa na kukataa tamaa, alijaribu kunywa maziwa yake mwenyewe bila mafanikio.

Necla anasema kwa mara nyingine alisikia sauti ya kitu kikichimba lakini sauti hizo zilisikika kwa mbali.

Amesema alifikiria mara kwa mara kuhusu familia yake, mtoto kwenye kifua chake, na mume na mtoto walipotea mahali fulani kwenye uchafu.


Necla amesema alitumia muda mwingi kulala na alipoamka alijikuta akilia, hivyo alilazimika pia kumyonyesha mwanaye aliyekuwa kifuani hadi atulie.

Baada ya zaidi ya saa 90 chini ya ardhi, Necla anasema alisikia sauti ya mbwa wakibweka kwa mara nyingine tena. Alijiuliza kama alikuwa anaota.

"Uko sawa? Gonga mara moja ndiyo," ilikuwa ni sauti ya mwokoaji aliyeita kwenye kifusi.

"Unaishi ghorofa gani?"

Waokoaji walichimba ardhini kwa uangalifu ili kumpata, huku naye aliendelea kumshikilia Yagiz kwa umakini.

Timu ya uokoaji kutoka Idara ya Zimamoto ya Manispaa ya Istanbul hatimaye walifanikiwa kuwaokoa yeye na mwanaye kisha kuwawahisha hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Alipofika hospitalini, Necla alilakiwa na wanafamilia waliomwambia kwamba mume wake, Irfan Kerim na mtoto wake wa miaka mitatu, Yigit Kerim, walikuwa wameokolewa kutoka kwenye vifusi.

Hata hivyo, wanafamilia hao walikuwa wamehamishwa hospitali katika Jimbo la Adana, wakiwa wamejeruhiwa miguu.

Mama huyo anaendelea na matibabu na imeelezwa kwamba hakuwa amepata majeraha makubwa na mwanaye.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad