Mabingwa Manchester City wamerejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu Uingereza baada ya kuwanyuka Arsenal 3-1 usiku wa Jumatano, Februari 15, kwenye Uwanja wa Emirates.
Vijana wa Pep Guardiola walionyesha ari yao ya kutetea taji la EPL kwa ushindi mnono uliowashuhudia wakipiku Arsenal kwa tofauti ya mabao.
Kevin De Bruyne ndiye aliiweka City kifua mbele katika kipindi cha kwanza kabla ya Bukayo Saka kusawazisha kupitia mkwaju wa penalti uliokuwa na utata.
Hata hivyo, winga Jack Grealish alifunga bao muhimu katika kipindi cha pili na kuwarejesha wageni uongozini.
Bao la Erling Haaland katika dakika za lala salama ndilo lilizamisha chombo cha Gunners.
Jinsi dimba lilipigwa
City walichukua uongozi wa mapema katika dakika ya 24 wakati Grealish alichuma nafuu kutokana na makosa ya Takehiro Tomiyasu ambaye alipiga pasi ya nyuma.
Grealish aliwasiliana na De Bruyne ambaye alivurumisha shuti kali iliyomwacha hoi mlinda lango Aaron Ramsdale.
Kisha Arsenal walisawazisha kupitia penalti iliyocharazwa na Saka dakika tatu kabla ya kipindi cha mapumziko.
Penalti hiyo ilitokana na Ederson kukimbia nje ya mstari wake na kugongana na mshambuliaji wa Arsenal kabla tu ya mpira kuondolewa langoni na Nathan Ake.
Katika awamu ya pili, faulo ya Gabriel dhidi ya Haaland iliamuliwa kuwa penalti lakini nyota huyo wa Norway alikuwa ameotea tu alipopokea pasi ya Kyle Walker hivyo uamuzi huo ulibatilishwa.
Hata hivyo presha ya City ilizaa matunda katika dakika ya 72 baada ya Haaland na Ilkay Gundogan kuwasiliana kabla ya kumumegea pasi Grealish ambaye alichonga ndizi hadi kimyani.
Haaland alipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Arsenal kunako dakika ya 82, akimalizia vyema krosi ya De Bruyne.
Wakijivuta nyuma ya Arsenal kwa pointi nane mwezi mmoja uliopita, Citizens wameshinda mechi nne kati ya tano zilizopita za ligi, huku Arsenal wakipoteza.
Lakini kinyang'anyiro hicho cha kuwania taji la EPL huenda kitafikia kilele wakati City watakua wenyeji wa Arsenal mnamo Aprili 26, 2023.
Juhudi za City kutetea taji lao zinakujia huku wakikumbana na hatari ya kushtakiwa kwa ukiukaji wa sheria zake za kifedha kati ya mwaka 2009 na 2018.
"Sawa, sasa tuko juu ya ligi, lakini Arsenal wana mchezo mmoja mkononi. Kushinda au kupoteza, una michezo mingi ya kucheza, lakini bila shaka kuja hapa na kushinda dhidi ya timu hiyo ni nzuri," Guardiola alisema baada ya mchezo huo wa Jumatano.
Huku wakiwa katika harakati ya kuwania taji lao la kwanza la EPL tangu mwaka wa 2003-04, Arsenal wameshindwa kuwazima City.
Arsenal chini ya ukufunzi wa Mikel Arteta, wamekosa kutwaa ushindi katika michezo yao minne walioshiriki katika mashindano yote, huku wakipoteza kwa City kwenye Kombe la FA kabla ya kupigwa na Everton na kutoka sare siku ya Jumamosi dhidi ya Brentford.