Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura, amesema kuwa Jeshi la Polisi limefanya uchunguzi na kuona upo umuhimu wa kurekebisha mfumo wa utoaji wa leseni za udereva ili kudhibiti ajali za barabarani.
IGP Wambura ametoa kauli hiyo baada ya kufanya kikao na wakuu wa polisi wa usalama barabarani wa mikoa yote Tanzania, wakaguzi wa magari na watahini wa madereva hii leo Februari 21, 2023 jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimelenga kuwakumbusha mambo ya kuzingatia katika utendaji kazi, usimamizi, ufuatiliaji na kuona namna bora ya kuondokana na ajali za barabarani ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji wa leseni za udereva.
Hii ni sambamba na kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa magari na watahini wa madereva wapya ambao watapewa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu