KIUNGO mshambuliaji wa Yanga raia wa Ghana, Bernard Morrison, amerejea kikosini baada ya kutatua matatizo yake na uongozi pamoja na benchi la Ufundi chini ya Kocha Nasraddine Nabi, ambapo ametakiwa kutofanya kosa lolote ndani ya miezi mitatu na ataanza kutumika kwenye mechi zijazo.
Morrison alikua nje ya kikosi hicho baada ya kwenda kwao Ghana kutatua matatizo yake ya kifamilia ambapo baada ya kurejea aliingia kwenye mgogoro mzito na uongozi na kutakiwa kufidia malipo ya pesa kwa muda wote aliozidisha baada ya kupewa ruhusa yake.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Championi Jumatano kwamba, tayari Kocha Nabi kamruhusu Morrison kuungana na wenzake kwenye kikosi cha kwanza ambapo ataanza kumtumia kwenye michezo ijayo ila hatakiwi kuonyesha kosa la utovu wa nidhamu ndani ya miezi mitatu ijayo.
“Uongozi kwa sasa umeshajua namna ya kuwabana wachezaji watukutu ambapo baada ya Morrison kuzidisha muda wa ruhusa aliyopewa kwenda kwao, ulimtaka alipie siku zote alizozidisha ambazo ni zaidi ya siku 14, jambo lilomfanya kocha na benchi la ufundi lote kumsimamisha kwenye kikosi cha kwanza.
“Tayari wamemalizana na kocha na sasa yupo kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu na Namungo, ambapo ametakiwa kubadilika na kutoonyesha jambo lolote la utovu wa nidhamu ndani ya miezi mitatu kama akiuka basi ataondolewa jumla kikosini na hilo limetolewa na benchi la ufundi pamoja na uongozi,” kilisema chanzo hicho.
Stori na Musa Mateja