Mwalimu mbaroni kwa kusambaza picha za wanafunzi





Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Mwalimu Elisha Chonya kwa tuhuma za kuwakalisha chini wanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Sinde na kisha kuwapiga picha na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii kwa madai kuna uhaba wa madawati.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewaambia waandishi wa habari Jumanne, Februari 7, 2023 baada ya kufika katika shule hiyo kujiridhisha.

“Taarifa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wanafunzi wakiwa wamekaa chini kwenye chumba kimoja cha darasa kwa madai ya uhaba wa madawati sio za kweli ni uzushi na kuwataka wananchi kuzipuuza kutokana na kuzua taharuki,”amesema.


Picha iliyosambaa mitandaoni ikionyesha wanafunzi wanasoma wakiwa wamekaa chini kwa madai ya kukosa madawati
Amesema kuwa kilichotokea na kuelezwa na Mwalimu  Mkuu, Anatalia Luwungo ni kwamba Februari 6, 2023 kulikuwa na kuandika majina kwenye madawati ya wanafunzi hivyo walilazimika kukaa nje kusubiria na ndipo mwalimu huyo alitumia fursa ya kuwaingiza  darasani kuwakalisha chini kisha kuwapiga picha na  kurusha mitandaoni.


“Hali hiyo imezua taharuki kubwa kwetu viongozi wa mkoa na kulazimika kufanya ziara ya kushtukiza kuja kujionea hali halisi, ambapo tumekuta wanafunzi wakiendelea na masomo na kuwepo kwa idadi kubwa ya madawati katika shule hiyo,” amesema Malisa.

Amesema kwa sasa Mtuhumiwa anashikiliwa na vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kujua lengo lake na nia ovu ya kuichafua Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju amekemea kitendo hicho na kuweka bayana kuanza kwa utaratibu wa kuwachunguza walimu  wa muda wa kujitolea wanataka kufundisha kabla ya kupata nafasi Serikali huku akishindwa kuweka bayana kama mwalimu huyo ni mwajiriwa au la.


“Kimsingi tukio hilo limeleta taharuki kubwa kwa sababu hakuna uhaba wa madawati na hata vyumba vya madarasa, kwa sasa tumeliachia Jeshi la Polisi kufanya kazi yake kwa hatua zaidi,”amesema.

Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Triphonia Kisiga amekemea tabia hiyo na kuonya walimu kuepuka tabia ya kuisemea vibaya Serikali kwa maslahi yao binafsi na kwamba kwa sasa licha ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi pia amesimamishwa kazi.

“Kwa hatua za awali tumemsimamisha kazi kupisha uchunguzi kwani bado hatujajua lengo lake lilikuwa ni nini,”amesema.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Anatalia Luwungo amesema kuwa taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mwalimu huyo siyo sahihi na kwamba amekiuka kanuni na taratibu za taaluma ya ualimu.


“Uhalisia ni kwamba Jumatatu Februari 6, 2023 kulikuwa na kazi kwa kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza kuandikiwa jina kwenye dawati,” amesema.

Mkazi wa Kata ya Sinde Jijini hapa, Sekela Saimon amesema kuwa kitendo hicho ni kuidhalilisha Serikali kwani kama jamii inashuhudia kazi kubwa inayofanywa na Mbunge wa Jimbo la Mbeya, Dk Tulia Ackson akichangia miundombinu ya shule na madawati kwa shule za sekondari na msingi.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad