Shabani Saidi Matola mkazi wa Kata ya Likongowele wilaya ya Liwale mkoani Lindi, amemuua baba mwenye nyumba wake aitwaye Siamini Rashidi Mtopoka (40), baada ya kumpiga na panga kichwani katika ugomvi unaolezwa kila mmoja akigombea alipwe fedha zake.
Imeelezwa kuwa mwenye nyumba alimfuata mpangaji wake kumdai pesa ya pango na mpangaji huyo alikataa kutoa akimtaka amlipe kwanza fedha zake anazomdai kutokana na kazi aliyokuwa amempa ya kubangua korosho.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Katani humo na kuthibitishwa na uongozi wa Kata husika na mamlaka ya kulinda usalama wa raia na mali zao mkoani Lindi, zinaeleza kuwa mauaji hayo yametokea Februari 5 mwaka huu 2023.
Mashuhuda wameeleza kuwa kauli ya mpangaji ya kutaka alipwe kwanza deni lake haikumfurahisha mmiliki wa nyumba hiyo na kuchukua uamuzi wa kumfungia mlango kwa nje na kuelekea ofisi ya afisa mtendaji wa Kata kwa lengo la kumshitaki mpangaji wake kukataa kumlipa fedha zake.
Walisema wakati mmiliki akiwa njiani kuelekea ofisi ya Mtendaji wa Kata,mpangaji alifanikiwa kuvunja mlango na kutoka nje na kumfuata baba mwenye nyumba wake akiwa na panga mkononi na alipomkuta alimpiga panga la kichwa,kisha kuanguka chini na kufariki papo hapo.
Mashuhuda hao wamesema kutokana na kitendo hicho, wananchi walimfuata kumkamata mpangaji Shabani na kumuweka chini ya ulinzi wao na kutoa taarifa Polisi,kituo cha Liwale mjini ambao walifika na kumchukua mtuhumiwa na kumfikisha kituoni kuendelea na taratibu zingine za kisheria.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo ya Likongowele,Augustino Godson Mbogo alipoulizwa amekiri kutoke mauaji hayo na kueleza tayari mtuhumiwa amekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kwa hatua zingine za kisheria.
Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Kamishina Msaidizi wa Polisi Pili Mande, alipoulizwa kuhusu mauji hayo amekiri na kueleza tayari mtuhumiwa Shabani Matola amekamatwa kwa mahojiano na watamfikisha Mahakamani muda wowote, baada ya uchunguzi wao utapokamilika.