Shirika la Urejeshaji Mali nchini Kenya limefutilia mbali kesi ya Tsh 40 bilioni dhidi ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Tebby Wambuku ambaye alipewa fedha hizo kama zawadi na mpenzi wake kutokea Ubelgiji miaka miwili iliyopita.
Mwanafunzi huyo alipokea pesa hizo mnamo Aprili 2021 kutoka kwa Marc De Mesel, raia wa Ubelgiji, ambaye pia alisambaza zaidi ya Tsh 105 bilioni kwa wanawake wengine watatu wa Kenya.
Waliopata fedha hizo ni Dada yake Wambuku, Jane Wangui Kago, rafiki yake Felista Nyamathira Njoroge na Sarah Wambui Kamanda.
Mamlaka ya kuchunguza umiliki wa mali kwa njia isiyo halali (ARA) ilifunga akaunti ya mwanamke huyo kwa madai kwamba huenda alikuwa anahusika katika upangaji wa mashambulizi ya kigaidi kwa kutumiwa pesa hizo nyingi kwa mkupuo.
Amana katika akaunti zake hazikuonyesha chanzo kingine chochote cha mapato kando na pesa zilizopokelewa kutoka kwa Bw De Mesel, hivyo kupelekea ARA kuhisi kuwa pesa hizo zilikuwa za uhalifu.
Ndipo ARA ilikimbia kortini na kupata maagizo ya kufunga akaunti ya benki ya mwanafunzi huyo kwa tuhuma kwamba fedha hizo hazikuwa halali.
Hata hivyo, wamekuja kuamua kuondoa shauri hilo mahakamani baada ya uchunguzi kuonyesha hakuna dalili zozote za uhalifu.
“Tuliitaka mahakama kuruhusu kesi hiyo iondolewe, uchunguzi haukupata ushahidi wa kutosha kuendeleza kesi ya kutaifisha. Tuna idhini iliyotiwa saini na pande zote mbili kutaka kesi hiyo iondolewe,” Wakili wa ARA Mohamed Adow aliambia mahakama.