KIKOSI cha Yanga jana usiku kilishuka uwanjani kutupa karata ya kwanza ya mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine alilala kisha akaamka na akili kubwa ya kama baba mlezi kwa kuamua kumtwangia simu kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Kocha huyo amefichua amemtwangia simu kiungo huyo aliyetangaza kuvunja mkataba na klabu hiyo, kisha Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini, kumzuia kwa kueleza bado ni mali ya Yanga, kisha akaanika mazungumzo yao yaliyotumia dakika 43.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Tunisia alipo na timu, Kocha Nabi alisema akiwa kama baba hafurahii maisha ya Fei Toto, hivyo alilazimika kumpigia simu siku chache kabla hajaondoka nchini kwenda Tunis.
Nabi alisema katika mazungumzo yake na Fei Toto amemtaka kiungo huyo kuifikiria kesho yake kwa upana na hatua ya kukaa nje maisha ya Yanga yataendelea lakini atapoteza makali yake na kufifisha kipaji chake.
“Mimi ni baba namchukulia Fei au mchezaji yeyote niliyenaye kama mwanangu wa kiume Hedi, ukiangalia Yanga maisha yanaendelea, lakini maisha ya Feisal yamesimama na kipaji chake kimesimama,” alisema Nabi na kuongeza;
“Nilimpigia, lakini niliongea na wachezaji wenzake nikamwambia kitu kikubwa sasa sio pesa tu anatakiwa pia kufikiria kuhusu kipaji chake, mtu bora ambaye atakuwa anamshauri vizuri ni yule atakayemwambia atafute nafasi ya kumaliza utofauti wake na klabu arudi kazini.
“Nafahamu athari za mchezaji kukaa nje bila kucheza mechi za mashindano, athari za mamna hiyo anaweza asizijue kwa undani mtu mwingine ambaye hachezi mpira wala hajacheza mpira, hata kama Feisal anataka kuondoka Yanga hiki kinachoendelea hakiwezi kumsaidia kitamuangamiza.”
Nabi aliongeza katika tamati ya mazungumzo yao Fei Toto alimuelewa na kumuahidi kurejea kazini wakati wowote atakapomaliza kuwasiliana na viongozi wa klabu hiyo.
“Aliniambia amenielewa akanishukuru na kuniahidi, kitu kikubwa nilichomshukuru Mungu ni kuniambia atarejea kazini atapomaliza kuongea na viongozi wa klabu, hili jibu lilinifurahisha sana naamini atafanya kweli, naamini hata wachezaji wenzake na mashabiki watampokea,” alisema Nabi na kuongeza;
“Kitu ambacho watu wanashindwa kukiona kwa mbali, hili sakata la Feisal sio tu Yanga inapoteza kitu lakini watu hawaoni hata timu ya taifa itapoteza nguvu muhimu, vipi leo inakuja mechi ya kimashindano ya Timu ya Taifa ya Tanzania na Feisal anakuwa nje?
“Nilimwambia Feisal asiangalie fedha za hapa leo angekuwa ndani ya kikosi angefikiria jinsi gani atajiuza kimataifa ambako huko kuna fedha zaidi na ndio msingi wa hizi mechi kuonyeshwa moja kwa moja ili dunia ione vipaji.”
Fei alipotafutwa jana na Mwanaspoti ili kutoa uffanuzi juu ya taarifa hiyo, siku yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe wa sms aliishia kusoma bila kujibu.