Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani hapa lina washikilia watu wanne kufuatia tukio la vijana wanaodhaniwa kuwa ni wa kundi la Panyarodi kuvamia makazi katika eneo la Bunju B Mtaa wa Idara ya Maji saa 8 usiku wa kuamkia leo Februari 10, 2023.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dr es Salaam, Jumanne Muliro amesema kundi la watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya wanane, walifika kwenye mtaa huo wakipiga kelele za mwizi, mwizi, ambapo nyumba zilizokuwa zinafungua wakifikiri ni wezi walikuwa wakivamiwa na kujeruhiwa.
“Ni kweli tukio kama hilo lipo kikundi cha wahalifu walivamia kwenye mtaa huo, kama unavyojua nyumba moja ya kupanga makuwa na familia zaidi tano, sio nyumba nyingi zilizovamiwa kama wanavyoeleza.
“Kwa wale waliofungua walijeruhiwa huku wakiwaamuru watoe fedha na wale wasiotoa walijeruhiwa maeneo mbalimbali ya na kusababisha watu nane kupata majeraha ambapo waliikimbizwa hospitali,” alisema Muliro.
Kamanda Muliro amebainisha kuwa pamoja na watu kujeruhiwa vijana hao walisababisha uharibifu ikiwemo kupasua runinga kwa watu wasiokuwa na fedha.
“Baada yaku kupiga kelele vijana hao walichukua bajaji na kukimbia lakini baadae walikimbizwa na bodaboda, walipofika njiani waliruka na kukimbia, polisi walifika na kuanza msako ambapo vijana wanne walikamatwa, ingawa wawili walijeruhiwa vibaya.
“Upelelezi wa awali unaonyesha vijana hao wametoka Mkoa wa Pwani tunaenelea na uchunguzi. Tunawashauri viongozi wa mitaa hiyo kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi,”alisema.
Mmoja wa majirani, Grace John ambaye nyumba yake haikuvamiwa alisema wavamizi hao walikuja majira ya saa 7 hadi saa 8 za usiku na walivamia nyumba za watu na kuwapiga mapanga.
“Tulisikia kelele za watu usiku, lakini hatukutoka nje, lakini baadaye tumeona majirani wakiwa wameumia kwa kushambuliwa na mapanga,” alisema.
Kwa upande wake mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Mama Munuo amesema watu hao walivamia majira ya saa 8 usiku na walivunja milango ya nyumba na kuingia na kuanza kukata watu mapanga.
Baadhi ya majeruhi katika tukio hilo wamelazwa hospitali ya rufaa ya Mwananyamala Kinondoni.