Wakala wa Christian Atsu ametangaza taarifa za kuvunja moyo baada ya kupatikana kwa pea mbili za viatu vya Atsu kwenye kifusi nchini Uturuki.
Mchezaji huyo wa zamani wa Newcastle na Chelsea alionekana mara ya mwisho akiwa nyumbani kwake huko Kahramanmaras ndani ya jengo ambalo liliangushwa na tetemeko la ardhi.
Kupitia mtandao wa Twitter, Wakala Nana Sechere amesema ”nipo kwenye eneo lilipokuwa jengo alilokuwa akiishi Atsu, nipo na familia yake, tukiendelea kumtafuta, mpaka sasa tumefanikiwa kulipata eneo sahihi kilipokuwa chumba chake na tumepata pea mbili za viatu vyake”
Itakumbukwa kuwa muda mchache baada ya kutokea kwa tetemeko hilo taarifa zinazosadikiwa kutolewa na Makamu wa Rais wa klabu ya Hatayaspor aliyokuwa akiichezea zilisambaa kwa kasi Kimataifa zikieleza kuwa Atsu amepatikana akiwa na majeraha.
Hata hivyo siku moja baadaye wakala wake alitoa taarifa kuwa hana mawasiliano yoyote na mchezaji huyo na anaendelea kumtafuta.
Mkanganyiko huu wa taarifa umeleta mgogoro mkubwa kati ya klabu ya Hatayaspor na wakala wa Atsu.
”Uokoaji unakwenda taratibu sana, msaada mkubwa bado unahitajika, pia tunahitaji watafsiri wa lugha, inasikitisha klabu yake hawapo hapa kusaidiana nasi” aliongeza Sechere.