Pinda Asema Sheikh Alhad Anastahili Udaktari wa Heshima





Dodoma. Wakati kukiwa na mjadala kuhusu utolewaji wa shahada za udaktrari wa falsafa wa heshima (PhD), Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ametetea shahada kama hiyo aliyopewa Mwenyekiti kamati ya maridhiano Sheikh Alhadi Mussa Salum, akisema anastahili kuwa nayo.

Alhadi Mussa Salum aliyekuwa Sheikh mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya kutenguliwa Februari 2 mwaka huu, alitunukiwa shahada hiyo Januari 2022 kwa kutambua mchango wake hasa kwenye suala la umoja na maridhiano.

Mjadala wa shahada hizo umeibuliwa bungeni wiki iliyopita kufuatia kuwepo ongezeko la baadhi ya wabunge walionazo, hatua iliyosababisha Serikali kutoa tamko ikisema haifuatilii taasisi au vyuo vinavyozitoa.

Akizungumza leo Februari 15, 2023 jijini hapa na viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania (JMT) ambayo kwa sehemu kubwa inaundwa na viongozi wa dini, Pinda amesema kuna mtu alimuuliza kuhusu shahada hiyo baada ya kelele nyingi kuhusu watu waliotunukiwa, ndipo akamjibu kuwa kiongozi huyo wa dini aliipata kwa halali na alistahili kupata.


"Baada ya kelele kidogo kuhusu watu kuhoji namna watu fulani fulani wanaotunukiwa PhD, nilimjibu kuwa yule aliipata kihalali na wala haikuja kwa njia za kona kwa hiyo huyu ni daktari," amesema Pinda.

Kuhusu Jumuiya ya Maridhiano amewataka kusimama imara katika kuzuia mmomonyoko wa maadili na kuzuia mifarakano badala ya kusubiri ichipue ndipo wakaanza kuitafutie suluhu.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu na ambaye ni mwanziliaji wa Jumuiya hiyo, amewataka viongozi kujikita katika kutafuta ufadhili ikiwemo ili kusaidia ujenzi wa zahanati Vijijini ambazo zitakuwa msaada mkubwa wa kusaidia watu waliopatwa na madhira.

Amesema katika kipindi cha miaka saba ambayo Jumuiya imeanza kufanya kazi, ameridhishwa na utendaji wao na ushauri wanaotoa kwa jamii katika suala zima la amani hiyo kazi yao itaungwa mkono.

Awali Sheikh Alhadi alizungumzia uwepo wake katika nafasi hiyo hata baada ya kupoteza nafasi yake ya Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema hilo halimzuii kwenye jukumu la amani la Taifa.

"Ni kweli lakini kabla ya hapo nilikuwa kiongozi wa mkoa, lakini haina kizuizi, nimeacha hiyo na ninaendelea kutumikia nafasi ya Kitaifa kwa hiyo kazi hii nakwenda nayo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad