Raia wa Nigeria Akamatwa na Mashine ya Kuchapisha Pesa Mapinga Bagamoyo




Bagamoyo. Maofisa Uhamiaji mkoa wa Pwani wamewakamata raia wawili wa Afrika Magharibi wakiwa na karatasi za kuchapisha pesa bandia, kemikali na kasiki (safe) la kutunzia fedha.

Watu hao wamekutwa pia na hati za kusafiria 34 za nchi za Nigeria na Ghana.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa huo, Abubakar Kunenge, amewataja watu hao waliokamatwa eneo la Mapinga, Bagamoyo, kuwa ni Livingstone Ese Onayomake (raia wa Nigeria) na Bertrand Noubissie (raia wa Cameroon).

Kunenge amesema Februari 9, 2023 walipokea taarifa za kiintelijensia kuhusu watu wanaotiliwa mashaka na siku iliyofuata ulifanyika upekuzi na kuwakamata raia hao.


Amesema wakati wa upekuzi mtuhumiwa Onayomake alikutwa na paspoti 34 ambazo si zake, kati yake 32 ni za Nigeria na mbili za Ghana.

Kunenge alisema alipohojiwa, mnaijeria huyo alidai alichukua paspoti hizo kwa lengo la kuwatafutia wahusika viza ya Uturuki.

"Jambo la kusikitisha raia hao walikutwa wakihifadhiwa na mtanzania, na mbaya zaidi mmoja alishaanza kujihusisha na utengenezaji wa fedha bandia maana alikutwa karatasi zilizoandaliwa kwa ajili ya kuchapisha noti bandia, kemikali pamoja na kasiki (safe) la kutunzia fedha,"alisema Kunenge.


Afisa uhamiaji Mkoani Pwani, Omary Hassan amesema baada ya kupata taarifa walienda kufanya upekuzi maungoni na kwenye makazi waliokua wakiishi.

Hassan ameeleza wahamiaji hao walikua wakiishi nyumbani kwa New Era Nyirembe ambaye alikua mke wa mtuhumiwa Noubissie, kwa sasa marehemu.

Amesema wamebaini kufuatia uchunguzi wa awali kuwa Onayomake aliingia nchini Februari 11 mwaka 2020 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kupewa viza ya matembezi ya siku 90 hadi Mei 05 mwaka 2020 lakini baada ya hapo ameendelea kuishi nchini kinyume na sheria hadi alipokamatwa

"Kuhusu Noubissie raia wa Cameroon yeye amekutwa na paspoti yenye namba 0441270 iliyotolewa Cameroon April 12, 2016 na iliisha muda Aprili 12 2021 na aliingia nchini mara ya mwisho Novemba 2, 2019 kupitia uwanja huo huo na alipewa viza ya matembezi iliyoisha Februari 01, 2020," amesema Hassan


Kufuatia tukio hilo, Kunenge ametoa rai kwa wananchi mkoani Pwani kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi waonapo watu wanaowatilia mashaka.

Pia amewataka raia wa kigeni kuhakikisha uwepo wao nchini unazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad