Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kufuatia vifo vya watu 17 vilivyotokea usiku wa kuamkia leo eneo la Magila Gereza, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Rais Samia ametuma salamu hizo leo Februari 4, 2023 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii huku mpaka sasa ikifahamika kuwa wanafamilia 14 wamefariki katika ajali hiyo.
“Nimesikitishwa na vifo vya watu 17 vilivyosababishwa na ajali iliyotokea jana saa 4:30 usiku, nawapa pole wafiwa na wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka,” ameandika Rais Samia.
Taarifa iliyotolewa leo alfajiri na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba imeeleza kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 17 na majeruhi 12.
Amesema ajali hiyo imetokea usiku katika eneo la Magira Gereza Kata ya Magira Gereza Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe, barabara ya Segera - Buiko.
"Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali yetu ya Wilaya ya Korogwe na majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na majeruhi wawili wamebaki Hospitali ya Korogwe kwa matibabu,” alisema Mgumba.
Ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar kwenda Moshi kwenye mazishi ambapo chanzo cha ajali hiyo kimetajwa kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva Fuso.