Jambo lililotokea kati ya Yanga na mdhamini wao mkuu naona ni makosa ya kiutendaji zaidi.
Hizi klabu kila siku zimekuwa zikihubiri mabadiliko ya kiuendeshaji, wanasema wamefanya mabadiliko na kutengeneza mifumo mipya ya kuendesha klabu kwa weledi.
Wamekuja na watu wanaoitwa CEOs [Watendaji wa Wakuu wa klabu], mimi ninachokiona kwa picha ya nje wametenegeneza tu structure kutuonesha uongozi umekamilika.
Tena wameajiri watu kutoka nje ya nchi ambao tunaamini ni watu waliobobea kabisa kwenye masuala ya weledi ili kuja kutusaidia kwenye masuala ya uendeshaji wa klabu kwenye mambo ya utendaji wa kawaida.
Lakini yanayotokea yanatuonesha picha nyingine kuwa hao watu hawapo, wapo tu kwenye picha! Hawapo kwenye utendaji wa kawaida kutokana na haya makosa yanayojirudiarudia.
Mtendaji Mkuu na watu wa idara ya sheria ndio watu wanaowajibika na hili tunaloliona. Inawezekana kwenye picha ya juu tunamuona Rais wa klabu au Makamu lakini kiuhalisia wao sio watendaji.
Rais wa timu inawezekana hajui mambo ya sheria na mikataba lakini Mtendaji Mkuu ndio anajua mikataba yote ya washirika wao na wanapaswa kuwapa nini na wao wanapata nini.
Yanga wanasema waliwasiliana na mdhamini mkuu wakampa mapendekezo akaridhia, wao wakaendelea na mchakato.
Saa chache baada ya mdhamini mwingine kutangazwa na kukaa kifuani kwenye jezi, anaibuka mdhamini mkuu anatoa taarifa ya kulalamikia kitendo kilichofanyika.
Aliyetoa taarifa ya Yanga kuwasiliana na mdhamini mkuu ni Rais wa klabu ambaye kiuhalisia si mtendaji! Kiuhalisia Mtendaji Mkuu ndio anawasiliana na mhusika [mdhamini mkuu].
Rais anapotoka kuzungumza na umma tayari anakuwa amepewa miongozo/ripoti na Mtendaji Mkuu, Rais anapotoa taarifa halafu baadae inalalamikiwa na mshirika wao maana yeke watendaji ndio wanaotakiwa kuwajibika.
Mimi naona hili jambo linapaswa kujibiwa na Mtendaji Mkuu pamoja na mwanasheria wa klabu. Mtendaji Mkuu ndio atuambie nani kawaingiza chaka?