Shule Zilizofanya Udanganyifu Kuchunguzwa



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, amemuagiza Kamishna wa Elimu kufanya uchunguzi wa kina kwa shule nne zilizobainika kufanya udanganyifu mkubwa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022.


Prof. Mkenda amesema hayo alipokutana na wazazi na walezi wa wanafunzi waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2022 wa shule ya sekondari Thaqaafa ya jijini Mwanza kwa ajili ya kuwasikiliza.


Amezitaja shule hizo kuwa ni Cornelius ya Kinondoni Dar es Salaam,  Thaqaafa ya Mwanza,  Mnemonic ya Zanzibar na Twibhoki iliyoko Mara na kumtaka Kamishna huyo kuchukua hatua kali kulingana na ripoti ya uchunguzi huo.


"Tunapowapeleka watoto shule tunataka wajifunze waelewe ili baadae waje watumikie taifa, sasa mtu anakuja kuwa daktari au mhandisi au rubani kwa kuiba mtihani, madhara yake ni makubwa sana," amesema Profesa Mkenda.


Mkenda amewapa pole wazazi na kuwataarifu kuwa mitihani hiyo imefutwa na  hivyo kilichopo ni kurudia mitihani. 


"Kuhusu kurudia mtihani tumewasikiliza  maombi yenu, ninashukuru kuwa hamna anayesema ameonewa sote tunakubaliana kuwa kulikuwa na udanganyifu  na hivyo niseme matokeo yamefutwa na kikubwa ni maombi ya kurudia mtihani, hili tunalichukua tutawasiliana nanyi baada ya kulifanyia kazi kwani ni suala la kibajeti pia," amefafanua Profesa Mkenda.


Naye Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akiwa katika kikao hicho amesema serikali haitalea shule zinazofanya udanganyifu wa mitihani na kuongeza kuwa wanafunzi wanatakiwa wapimwe kwa uwezo na sio kwa kudanganya.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad