Kocha, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amefichua namna alivyojipanga kwa mechi dhidi ya AC Horoya, akisema tangu walipocheza mechi ya Ligi Ku dhidi ya Singida Big Stars walipata wasaa wa kuisoma kupitia video na sasa huenda akabadili mfumo watakapowakabili wenyeji.
Simba na Horoya zitaumana leo katika mechi ya kwanza ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mjini Conakry na Kocha Robertinho alisema; “Kuna baadhi ya mechi zao niliziona kupitia kanda za video na tuligundua vitu vingi kutoka kwao jinsi wanavyocheza wakati wanamiliki mpira na muda ambao hawana.
“Bahati nzuri hapa Simba kuna mtaalamu wa kuchambua wapinzani kupitia video, Culvin Mavunga tumefanya kazi nzuri kwa pamoja na kuanza maandalizi mapema. Baada ya hapo tulishusha kwa wachezaji kuanza kuvifanyia kazi vyote ambavyo tutavitumia mechi hii naamini mambo yatakuwa mazuri kwa upande wetu na kupata matokeo bora kama tunavyohitaji,” alisema Mbrazili huyo na kuongeza;
“Ukiangalia hali za wachezaji wote zipo sawa kila mmoja yupo na morali ya juu kuhakikisha Simba inaanza vizuri kwa kupata pointi katika mchezo wa ugenini na hilo linawezekana kutoka na maandalizi yetu.”
Winga wa Simba, Pape Sakho alisema wanakwenda kucheza mechi ngumu ila wachezaji wamekubaliana kila mmoja kwa nafasi yake kupambana ili timu ianze kwa matokeo mazuri.
“Wachezaji wenzangu wote ukiangalia baada ya mechi na Singida kila mmoja alikuwa anaizungumzia mechi na Horoya AC, kwa kiasi gani inaonyesha tunahitaji kuanza vizuri ugenini ili kujirahisishia kazi mapema,” alisema Sakho na kuongeza;
“Hata kwenye maandalizi yetu ilionyesha kiasi gani tunatamani kuanza kukusanya pointi mapema licha ya kuanzia ugenini kwenye michezo ambayo huwa na mambo mengi na ushindani wa kutosha kutoka kwa wapinzani.”