Simba Yalainishiwa kwa Raja, Yanga Mmh!

 


Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limefanya uamuzi unaoonekana kama neema kwa Simba katika mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casabalanca ya Morocco itakayopigwa leo Jumamosi kuanzia saa 1:00 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.


Uamuzi huo unaowalainishia wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo ni uteuzi wa mwamuzi mwenye nyota ya bahati kwa timu zinazocheza nyumbani kila anapokuwa akipuliza filimbi, Blaise Ngwa (41) kutoka Cameroon.


Kumbukumbu ya mechi za nyuma za michuano ya klabu Afrika zilizochezeshwa na refa huyo, inaonyesha mara nyingi timu mwenyeji imekuwa ikifanya vizuri kwa kupata ushindi, huku ikiwa ngumu kwa upande wa wageni.


Katika mechi 11 za michuano ya CAF refa Ngwa alizochezesha, timu zilizokuwa nyumbani zilipata ushindi mara nane, sare zikiwa mbili na mara moja tu ambayo timu ngeni ilipata ushindi. Hata hivyo, Simba inapaswa kuwa makini upande wa nidhamu, kwani refa huyo amekuwa na tabia ya kupenda kumwaga kadi ambapo katika mechi hizo 11 alizochezesha hapo nyuma, alitoa jumla ya kadi 49 za njano ikiwa ni wastani wa kadi 4.5 kwa mechi.


Mwamuzi huyo kwenye mechi hiyo ya kesho atasaidiwa na marefa wenzake watatu kutoka Cameroon ambao ni Elvis Nguegoue, Carine Artezambong na Jeannot Bito.


Wakati Simba ikipewa refa huyo wa bahati, kwa upande wa watani wao Yanga wamekutanishwa na refa mwenye nuksi na timu za nyumbani, Abdelaziz Bouh kutoka Mauritania kuchezesha mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.


Mechi hiyo ya Yanga na Wakongoman itapigwa keshokutwa Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku kumbukumbu zikionyesha kuwa Bouh (30) katika mechi sita za michuano ya CAF alizowahi kuchezesha, timu zilizokuwa nyumbani zilipata ushindi mara mbili tu, zikitoka sare mara mbili na kupoteza mbili.


Katika mechi hizo sita ambazo refa huyo kutoka Mauritania alichezesha, alitoa kadi 20 zote zikiwa za njano ambazo ni wastani wa kadi 3 kwa mchezo.


Mwamuzi huyo atazihukumu Yanga na Mazembe akisaidiwa na raia wenzake wa Mauritania, Hamadine Diba, Brahim H’Made na Moussa Diou.


Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema wawakilishi wote wa Tanzania wasiingie na mawazo ya marefa vichwani kwenye mechi mwishoni mwa wiki hii.


“Wajiandae kwenda ndani ya uwanja kupambana na wasiwafikirie marefa. Wakitimiza wajibu wao, watafanya vizuri pasipo kujali marefa wanapendelea upande wa pili au wanachezesha kwa kufuata sheria za soka.


“Naamini Simba na Yanga wote wana timu nzuri na watatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata ushindi,” alisema Cannavaro.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad