Straika wa Al-Qadsiah, Mtanzania Simon Msuva anapambana kuhakikisha anaikwamua timu hiyo isishuke daraja, kutokana na nafasi ya 15 iliopo sasa, huku ikiwa imebakiza mechi tatu tu kufunga msimu, huku akitaka kufunga mabao 15.
Katika mechi 21 iliyocheza timu hiyo, imeshinda tano, sare saba, imepoteza tisa na imevuna pointi 22, ina jumla ya mabao 15, huku Msuva akifunga saba katika mechi saba sawa na kusema kuwa amefunga nusu ya mabao yote.
Ili Al-Qadsiah isishuke daraja inatakiwa ishinde mechi tatu zilizobakia, kwani timu tatu zilizopo chini yake ambazo ni Al Sahel ina pointi 20, Najran ina pointi 18 na Shoulla pointi 11.
Msuva alisema anajiona ana kazi nzito ya kuitetea timu yake, hivyo anahitaji kufunga mabao mengi zaidi na ikiwezekana amalize na mabao 15 ambayo yatakuwa yakiipa ushindi wa kupata pointi timu hiyo.
“Timu yangu haipo nafasi nzuri, hivyo naelekeza nguvu zangu, akili zangu zote nazipeleka hapa kuhakikisha nafunga mabao ya kupata pointi kwa maana timu ishinde na siyo sare ama kufungwa hiyo ndio itakuwa furaha yangu.
Aliongeza “Ndio maana natamani kufunga mabao mengi angalau nifikishe 15 kwa mechi zilizosalia, naamini kwenye dhamira hakuna kinachoshindikana na tabia yangu ni kutokukata tamaa kwa jambo lolote,” alisema mchezaji hiyo wa zamani wa Wydad Casablanca ya Morocco.
Alisisitiza hataki historia ya kushuka na timu, badala yake anatamani kuandika rekodi ya kukumbukwa huduma yake :”Natamani nifanye vitu vya kuacha alama kwamba alikuwepo Mtanzania alifanya kitu hiki kwenye timu, ndio maana naweka akili yangu kwenye hizo mechi tatu ili tubaki salama,” alisema.
Kabla ya Msuva kujiunga na Al-Qadsiah, timu nyingine za nje alizocheza ni Difaâ El Jadida (2017-2020) na Wydad (2020-2022) na Tanzania alizichezea Azam FC (2010/11), Moro United (2011/12) na Yanga (2012-2017)