Spika ataja sababu kukwama Muswada wa Bima ya Afya Kwa Wote



Wakati  Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHC) ukisubiriwa kujadiliwa bungeni, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameeleza sababu za muswada huo kutopelekwa bungeni leo kama ilivyokuwa imepangwa kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za mkutano wa 10 wa Bunge.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Muswada wa Sheria  Bima ya Afya kwa Wote (UHC), uliokuwa uwasilishwe leo bungeni umeshindwa kuwasilishwa kwasababu majadiliano kati ya Bunge na Serikali bado yanaendelea.


Akizungumza leo Februari 9, 2023, baada ya kipindi cha maswali na majibu, Dk Tulia amesema majadiliano bado yanaendelea kwa lengo la kuuboresha zaidi muswada huo hasa katika eneo la mambo yanayohusu bajeti ama yanayohusu fedha.


“Wabunge muswada huu wa mwaka 2022 utawasilishwa wakati mwingine kamati itakapokuwa imekamilisha kujadiliana na Serikali kwenye mambo ya kifedha,” amesema Dk Tulia.


Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge iliyotolewa Januari 30, 2023, ulionyesha kuwa muswada huo ulikuwa uwasilishwe bungeni leo kwa hatua zake zote tatu za mchakato wa utungwaji wa sheria.


Hii ni mara ya pili kwa muswada huo kukwamba tangu usomwe kwa mara kwanza bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge na kupelekwa katika Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuchambuliwa.


Mkutano wa tisa wa Bunge, muswada huo ulipangwa kujadiliwa kwa siku moja Novemba 12 mwaka jana lakini ulikwama.


Akitoa ufafanuzi kwanini haukuwasilishwa muswada huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema muswada huo ulishindwa kusomwa mara ya pili kwasababu Serikali na Bunge bado lilikuwa likiendelea na majadiliano.


“Sasa hati hii haitawasilishwa leo mezani kwasababu Bunge pamoja na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri,”alisema.


Dk Tulia alisema Bunge lilikuwa likiendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na wabunge, wadau mbalimbali waliojitokeza katika kamati na nyingine Serikali.

Hata hivyo, Januari 20, 2023 Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema kazi ya uchambuzi wa muswada huo ilikuwa imekamilika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad