Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson amesema shahada za udaktari wa falsafa ‘degree za heshima’ zinazotolewa na vyuo au taasisi mbalimbali zilizo nje ya nchi kwa Watanzania hususani wabunge, athari zake zinaweza zisionekane sasa lakini zikaonekana baadae kwa Taifa.
Amesema Tanzania kupitia sekta ya elimu inajivunjia heshima kuona degree hizo za heshima zinazotolewa kwa gharama ya dola za Marekani 2500 na kugawiwa kama pipi kwa viongozi kwani ni jambo ambalo halikubaliki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Dk. Tulia ametoa kauli hiyo leo wakati akihitimisha muongozo uliotolewa na Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka kufahamu iwapo mamlaka ya elimu nchini inatambua vyuo hivyo hivyo vinavyotoa degree za heshima kwa viongozi nchini.
“Baadhi ya wabunge wana muda mfupi sana lakini wametunukiwa, wapo wenye miaka mingi hawajabahatika kutunukiwa. Ni vigezo gani vinatumika kuwatunukia na ni kwa kiasi gani mamlaka zinazosimamia elimu zinatambua udaktari huu,” amehoji Shangazi.
Dk. Tulia amesema degree za heshima zinazotolewa mathalani kwa Rais Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, vyuo vimefanya utafiti kuhusu kazi alizozifanya sio tu alipokuwa rais bali tangu aanze kufanya kazi.
Amesema kwa upande wa Rais Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), huzikusanya taarifa hizo na kuzipima kwa vigezo walivyoviweka kwamba katika vigezo hivi rais wanaweza kumtunuku degree ya falsafa ambayo amepewa au lah.
“Sasa tutafika mahali ambapo wale wanaopewa kwa heshima wanayostahili hawana tofauti na hawa wanaolipa pesa wapewe hizo degree. Sisi kama Taifa lazima tufahamu utaratibu upi tunataka kwenda nao kwa sababu tusipofanya hivyo tunajipoteza wenyewe.
“Viongozi lazima tuoneshe mfano, mtoto wako umempeleka shule ili asome atie bidii, leo wewe kama mzazi unalipa pesa ili upewe degree ya heshima, unampa mfano gani yule kijana aliye shule unayemkazania kusoma? kwamba na wewe tafuta pesa ukipata kalipe na wewe utapewa degree” amesema Spika Dk. Tulia.
Aidha, amesema mchakato huo hauna uhusiano na wale waliopewa au kulipa ili wapatiwe degree hizo za heshima.
“Vyuo vinavyotambuliwa havitoi degree kila wiki, kila mwezi, kila siku kila mwaka, kafuatilieni UDSM, UDOM kimetoa degree za heshima kwa watu wangapi, sio hivi vya nje vitumwagie degree za malipo alafu vya ndani havioni mchango wetu,” amesema.
Amesema ni muhimu kwa viongozi na Taifa kuweka muongozo mzuri kwa ajili ya viongozi wanaofuata baada yao.
Amesema kwa kuwa Tanzania sio kijiji bali sehemu ya dunia nzima, hivyo vyuo au taasisi hizo zinazogawa degree za heshima zingeanza na nchi zao kugawia kila mtu degree.
“Nilishawahi kupata ujumbe kutoka kwa daktari wa kisomo, alisema tunapoeleka nadhani nitaandika barua niache kutambuliwa kama daktari kwa sababu hana tofauti na huyu aliyetoa dola za Marekani 2,500 kulipia kile cheti,” amesema.
Amesema lazima Tanzania ioneshe mfano mzuri kama Taifa hata kama waziri amesema hawajaombwa kufanya uhakiki kwani uhalisia wote unafahamika namna degree za heshima zinavyotolewa.
“Hizi nyingine zinazoleta wageni kwa ajili ya kuleta makabrasha ya vyeti vya kugawia watu wakiuza kama pipi haikubaliki! tunajivunjia heshima kama Taifa hasa kwenye eneo letu la elimu lakini la kuwapa heshima kwa wanaostahili.
“Kwa kusema hayo, kwa sababu msimamizi wa sekta na amesema, hayawazuii kuendelea na utaratibu wenu lakini mchukue jukumu la kufanya kama viongozi ambao wenzenu wanawatazama nyuma na watoto wenu wapo shule na mngependa wasome mpaka kukuta kibao kimegeuka,” amesema.
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda mbali na kufafanua aina za shahada hizo, amesema hawajawahi kuombwa kuhakiki degree hizo za heshima wala vyuo vinavyotoa degree hizo kwa viongozi.
Amesema kuna namba tatu za kupata degree hizo ambapo ya kwanza ni kusomea darasani na kuandika chapisho la kitafiti na kutunukiwa na chuo kinachotambulika popote duniani, pili ni kujisajili kwenye chuo na kufanya utafiti huku ukisimamiwa bila kwenda darasa kisha kutunukiwa degree hiyo.
Joseph Kasheku ‘Msukuma,’ Mbunge wa Geita Vijijini
“Tatu ni hizi za heshima ambazo zinatolewa na ni utamaduni wa dunia nzima, kuna watu kwa michango yao ya aina mbalimbali chuo kinachotambulika kinaweza kumpa heshima kwa kutoa doctorate kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina utaratibu wake, ili mtu atunukiwe lazima itolewe proposal ndani ya chuo na mtu ambaye anatambulika ifanyiwe utafiti ihakikiwe ndipo wawasiliane na mtu anayetakiwa kupatiwa aende akapate,” amesema.
Amesema kuhusu viongozi wanaotunukiwa katika hivi sasa serikali ipo tayari kufanya uhakiki wa vyuo hivyo pale itakapoombwa kufanya hivyo kwani kwa sasa haiwezi kwenda kuhakiki kwa kia mtu aliyetunukiwa degree ya heshima.
Hayo yanajiri wakati kukiwa na mijadala kuhusu degree hizo za heshima hususani baada ya Disemba mwaka 2021, Chuo cha The American University USA cha nchini Marekani kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Siasa na Uongozi, Mbunge wa Geita vijijini Joseph Msukuma (CCM) na wenzie 15.
Aidha, tarehe 27 Januari 2023, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki ambaye pia ni Meneja wa Record Label ya wcb, Hamisi Taletale alitunukiwa Shahada ya udaktari wa heshima kutoka katika Taasisi ya Academy of Univeral Global Peace (AUGP-USA) ya nchini Marekani.