Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania
RAIS Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi Jumuiya wa Wanafunzi wa Elimu ya juu (TAHLISO) la kuongeza fedha za kujikimu kutoka Sh 8,000 hadi 10,000 kwa siku. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya Rais TAHLISO, Frank Nkinda kumuomba Rais Samia kuridhia kuongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi hao kutokana na gharama za maisha kupanda.
“Hali ya maisha imepanda, tunashukuru kwa kutupatia kiasi cha 8000 kwa ajili ya kujikimu. Kwa kuwa wewe kwetu ni mama na ni Rais lakini naomba nitumie kofia ya mama… ulezi wa taasisi hii na vijana wa vyuo vikuu, kiasi hiki kipande hadi 10,000 au zaidi itakavyokupendekeza,” amesema Nkinda.
Akijibu baada ya changamoto zilizowasilishwa na Nkinda katika mkutano wake na viongozi wa TAHLISO jijini Dodoma leo tarehe 11 Februari 2023, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ProfESA Adolf Mkenda kwenda kuanza na Sh. 10,000.
Aidha, wanafunzi wanaosoma ngazi ya cheti na diploma nao kunufaika na mikopo ya elimu ya juu, rais Samia amesema licha ya bajeti kutokuwepo kutokana na kazi zilizopo sasa, suala hil Serikali inafikiria kuweka kwenye mipango yake.
“Lakini nilikuwa nanong’nona na waziri wetu kwamba akajipekue vizuri, akipata kidogo na mimi nitajazie ili uweze kutoa. Kama tutashindwa mwaka huu, tuachieni mwakani,” amesema.
Awali Nkinda amesema “Kuna wadogo zetu wanasoma ngazi ya cheti na diploma, kwa sheria za sasa sio wanufaika na mikopo wa ngazi ya elimu ya juu, tunaomba mwaka wa fedha 2023/2024 wawe wanufaika wa mikopo ngazi ya elimu ya juu,” amesema.