Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), zinadaiwa kutupiana mpira kuhusu uchunguzi na mashtaka dhidi ya wanaodaiwa kuhujumu Chama cha Ushirika cha Usafirishaji Mruwia mkoani Kilimanjaro.
NPS inafanya kazi chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Uchunguzi wa tuhuma hizo zilibainishwa katika taarifa ya ukaguzi na uchunguzi wa chama hicho mwaka 2019, lakini tangu kutolewa kwa ripoti hiyo, hakuna mtu ambaye ameshitakiwa kwa ubadhirifu huo.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikes alisema jalada la uchunguzi wa suala hilo lipo kwa mwendesha mashitaka wa Mkoa kwa ajili ya mapitio kama sheria inavyotaka.
“File (jalada) lipo kwa mwendesha mashitaka wa mkoa, tumepeleka huko kwa mapitio kama sheria inavyotaka na yeye ndiye atatupa go ahead (ruksa) kama kesi inaenda mahakamani au nini kifanyike,” alisema Wikes.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jana, mwendesha mashitaka wa Kilimanjaro kutoka NPS, Nuda Khalili alisema jalada hilo tayari lipo Takukuru kwa ajili ya upelelezi zaidi, “hivyo hilo file liko kwao.”
Ukaguzi huo ulifanywa kwa maagizo ya Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Kilimanjaro kati ya Januari 1, 2002 na Juni 18,2018 na kubainika kuwepo kwa udanganyifu katika matumizi ya fedha benki.
“Udanganyifu huu wa kuzidisha matumizi kila mwezi hadi Juni 18, 2018 ulisababisha Petty Cash kuwa na matumizi ya ziada (Overdraft) ya jumla ya Sh99.6 milioni, na fedha hizo zilitolewa benki,”inaeleza taarifa hiyo ya ukaguzi.
Mbali na hilo, lakini taarifa hiyo ambayo gazeti hili inayo, inaeleza kuwa Sh9.6 milioni zilitolewa Mruwia Saccos, lakini Sh405,000 ndiyo ilipokewa katika vitabu vya Mruwia hivyo kuwepo upotevu wa Sh9.2 milioni.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa hadi Juni 2018, chama hicho kinaonekana kilikuwa kimekopa kutoka Mruwia Saccos Sh14.3 milioni lakini kati ya fedha hizo, Sh11 milioni kilinachoonekana kwenye vitabu hivyo kiasi cha Sh3.3 milioni hakikupokelewa.
Mwananchi