Tundu Lissu "Siungi Mkono Mapenzi ya Jinsia Moja"


Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema haungi mkono mapenzi ya jinsi moja, na kwamba angekuwa anaunga mkono basi angeweka wazi.

Lissu ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akihojiwa na moja ya vyombo vya habari nchini Tanzania ambapo alisema kuwa wenye utamaduni huo waendelee na utamaduni wao.

”Wenye utamaduni wao, waendelee nao. sisi wenye utamaduni tofauti, tuendelee na utamaduni wetu. Kwani sheria zetu zinaruhusu mapenzi ya jinsia moja? Haziruhusu. Tamaduni zetu zetu zinaruhusu mapenzi ya jinsia moja? Basi sisi tuendelee na utamaduni zetu…

„…Mimi sijawahi kusema mahali popote katika dunia hii kwamba naunga mkono mapenzi ya jinsia moja, hizo ni siasa za maji taka,” alisema mwanasiasa huyo.


Katika mahojiano hayo, Lissu alisema kuwa, kuhusishwa kwake na kusapoti mahusiano ya jinsia moja kulianza baada ya kushiriki mahojiano kwenye kipindi cha Hard Talk kinachorushwa na BBC.

'Serikali isiingilie faragha'

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema, alitoa rai kwa kusema Serikali haipaswi kuingilia mambo ya faragha ya mtu.

”Mambo ya faragha, serikali haitakiwi kuingilia. Tukiruhusu Serikali kuingia majumbani mwetu. Serikali maana yake ni polisi, usalama wa taifa na watu wa aina hiyo. Waje waone mnapojifungia vyumbani mwenu. Itakuwa ni nchi ya aina gani ambayo utakaa chumbani na mwezi wako mkapata faragha?” alisema Lissu.

Alisema, Nchi ina katiba na serikali hairuhusiwi chumbani na msimamo wake ni kuwa serikali haitakiwi kuingilia mambo ya faragha.


Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chadema ambaye mwaka 2020 alirejea nchini kutoka uhamishoni kuja kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa nchi ambapo alikuwa akiwania dhidi ya Rais, John Magufuli.

Lissu alipata asilimia 13 za kura, matokeo yaliyopingwa na chama chake kikidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa kwenye mchakato wote wa upigaji kura.


Baada ya uchaguzi huo kuisha, Lissu alirejea uhamishoni nchini Ubelgiji ambapo amekuwa akiishi muda mrefu uhamishoni kutokana na kile alichodai kuwa alikuwa akitishiwa usalama wake nchini Tanzania nyakati za utawala wa Magufuli.

Kwasasa, mwanasiasa huyo amerejea nchini na anaendelea na shughuli za kisiasa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad