Uchunguzi maji ya maiti kuhifadhi samaki waanza



HOSPITALI ya Rufani ya Kanda ya Bugando imeanza uchunguzi kubaini ukweli wa taarifa za maji ya kuhifadhi maiti kutumika kuhifadhi samaki.

Uchunguzi huo wa kisayansi unafanywa kufuatia agizo la Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango la kufanya utafiti kuhusu kinachodaiwa kuwapo ongezeko la magonjwa ya saratani mikoa ya Kanda ya Ziwa linalosababishwa na matumizi ya maji hayo kuhifadhi kitoweo hicho kinachotumiwa na wakazi wengi wa mikoa hiyo.

Utafiti huo unafanyika kupitia sampuli mbalimbali za wagonjwa wa saratani pamoja na wale wasiokuwa na ugonjwa huo wanaoishi Kanda ya Ziwa ili kubaini ukweli wa madai hayo kama alivyoamuru  Makamu wa Rais wakati wa uzinduzi wa wodi ya wagonjwa wa saratani hospitalini huko hivi karibuni.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani na Mkuu wa Idara ya Saratani wa hospitali hiyo, Dk. Nestory Masalu, alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani.

Bingwa huyo wa saratani alisema utafiti wao huo unatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita.


"Tayari tumekusanya sampuli 7,000 za watu wenye saratani mbalimbali pamoja na sampuli 7,000 za watu wasiokuwa na saratani, wote wakiwa na umri uleule na wanaishi mazingira hayo hayo ili tujue sababu za hawa kupata ugonjwa huo na wengine kutokupata ugonjwa huo," alisema Dk. Masalu.

Alisema kwa sasa tayari wana taarifa hizo na wanafanya uchambuzi wa taarifa hizo na majibu yake yanatarajiwa kutolewa baada ya miezi sita kutokana na ugonjwa huo kuchukua muda mrefu kuleta majibu sahihi.

Dk. Masalu alibainisha kuwa kwenye hospitali hiyo kwa sasa wanapokea wagonjwa wa saratani takriban 1,500 kwa mwaka, idadi inayoonekana kuwa kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2009.


Alisema kuwa tangu kuanza kutolewa kwa huduma hiyo hospitalini huko, wamefanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa wa saratani 55,000 huku wagonjwa 10,000 wakifariki dunia wakati wa matibabu.

"Ninatoa wito kwa wananchi hasa wale wenye umri mkubwa kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kukabiliana na ugonjwa huo mapema," alisema Dk. Masalu.

Baadhi ya mashuhuda waliopona ugonjwa wa saratani, waliungana na bingwa huyo kuwashauri wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kukabiliana na ugonjwa huo mapema pindi wanapogundulika.

"Nimefanyiwa upasuaji wa titi kutokana na ugonjwa huu na mpaka sasa hali yangu ni nzuri. Ninashukuru Mungu ugonjwa huu umepona.

"Kikubwa ni kuhakikisha unapima mapema ili kuepusha kukaa na ugonjwa huu ukafikia hatua ngumu kutibiwa," alisema Geredina Nzogela.

Katika maadhimisho hayo, Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando ilitoa huduma za upimaji wa magonjwa ya saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume na saratani ya matiti bila malipo.

Kwa muda mrefu kumekuwa na madai mengi kuhusu kasi ya ongezeko la saratani Kanda ya Ziwa, baadhi wakijihusisha na kemikali zinazotokana na migodi mingi iliyoko kwenye ukanda huo pamoja na kemikali zinazotumika kwenye kilimo cha pamba, tumbaku na kahawa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad