Unaambiwa Huko Yanga na Fei Toto Mambo ni Mazuri



HATIMAYE mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na kiungo, Feisal Salum 'Fei Toto' wamemalizana na nyota huyo mwenye asili ya Zanzibar anatarajia kurejea katika kikosi cha timu hiyo hivi karibuni, imefahamika.

Fei Toto alitangaza kuvunja mkataba wake na Yanga kwa kuilipa kiasi cha Sh. milioni 112 lakini shauri hilo lilipopelekwa katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliamuru nyota huyo bado ni mchezaji wa klabu hiyo ya mitaa ya Jangwani na Twiga.

Lakini pia limeonekana kumalizika ikiwa zimepita siku chache tangu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Ally Mayay, kuzitaka pande hizo mbili kukaa pamoja na kumaliza sintofahamu hiyo kwa kutumia busara.

Taarifa za uhakika zilizopatikana jijini Dar es Salaam kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema viongozi wa Yanga walikwenda Zanzibar kufanya mazungumzo na mchezaji huyo na kufikia makubaliano mapya.

Chanzo chetu kilisema baada ya mazungumzo hayo, wamekubaliana kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya Sh. milioni 350 na atalipwa mshahara wa Sh. milioni 15 kwa mwezi.


“Ni kweli kulikuwa na mvutano mkubwa sana hadi sakata hili kufika katika ngazi ya juu hadi serikali kuingilia kati, hatimaye sakata limefikia mwisho baada ya busara kutumika kwa pande zote mbili,” kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza baada ya kukamilisha makubaliano hayo mapya, sasa Fei Toto anatarajia kuingia kambini baada ya Yanga kumaliza mchezo wake wa mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Imeelezwa Yanga imefikia uamuzi huo ili kuongeza nguvu katika kikosi chake kwa ajili ya kuhakikisha wanafikia malengo ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA pamoja na kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.


Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, aliliambia gazeti hili nyota huyo anatakiwa kurejea katika majukumu ya klabu kwa ajili ya kulinda kipaji chake na manufaa kwa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Nabi alisema Fei Toto ni mchezaji wa kutegemewa wa Yanga na Taifa Stars na kumalizika kwa sakata lake ni jambo la faraja.

Fei Toto amekuwa nje ya kikosi cha Yanga tangu Novemba mwaka jana na presha ya madai yake ya kuboresha mshahara wake ilishika kasi zaidi wakati dirisha dogo la usajili lilipofunguliwa.

Katika muda ambao hakuwa na kikosi cha Yanga, Fei Toto, alionekana amekwenda Dubai kwa ajili ya mapumziko ya muda mfupi kabla ya kurejea nchini kusikiliza shauri lililokuwa linamkabili.


Mapema mwaka huu nyota huyo alionekana akifanya mazoezi na timu yake ya zamani ya JKU ambayo ilikuwa ikijiandaa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi huko Visiwani Zanzibar.

Simba na Azam FC zilitajwa kumwinda Fei Toto, lakini mabosi wa timu hizo mbili walikanusha kuhusika na mchakato wa kumshawishi Mzanzibari huyo kuondoka katika klabu yake.

Viongozi mbalimbali wa serikali walitajwa kuhusika katika kumshawishi Fei Toto kurejea katika klabu hiyo na kwa nyakati tofauti mchezaji huyo alikaririwa akisema atakuwa tayari kucheza kwenye timu itakayomlipa maslahi mazuri.

Katika kuhakikisha anapata haki yake, Fei Toto alilazimika kuomba marejeo ya kesi yake ambayo ilifunguliwa na Yanga.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad